Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR yataka vikwazo ziondolewe kusaidia wagonjwa wa COVID-19

OHCHR yataka vikwazo ziondolewe kusaidia wagonjwa wa COVID-19

Pakua

Wakati idadi ya wagonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 ulimwenguni ikizidi kupaa na kuwa zaidi ya 330,000 huku vifo vikifikia 1,4652, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet ametaka vikwazo vya kisekta duniani viondolewe ili mataifa yaweza kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo. Grace Kaneiya na ripoti kamili.
 
(Taarifa ya Grace Kaneiya)
 
Taarifa iliyotolewa leo mjni Geneva, Uswisi na ofisi ya yake, imemnukuu Kamishna Mkuu Bachelet akisema kuwa vikwazo hususan katika sekta ya afya vinaweza kusababisha maambukizi na vifo zaidi na hata kusambaratisha mifumo ya afya.
 
“Misingi ya kibinadamu inapaswa kuzingatiwa kwenye vikwazo hivyo haraka hususan kwenye vifaa vya matibabu na dawa,”  amesema Bi. Bachelet akitolea mfano Iran ambako amesema watu wapatao 1,800 wameshafariki dunia kutokana na COVID-19 kwa sababu vikwazo vinakwamisha wao kupatiwa vifaa kama vile vivutia hewa na vifaa vya  kusaidia wahudumu wa afya kujikinga dhidi ya virusi.
 
Bi. Bachelet amesema zaidi ya madaktari 50 wamefariki dunia nchini Iran tangu wagonjwa wa awali wathibitishwe nchini humo wiki 5 zilizopita, “janga la Corona linasambaa nchi jirani na litakuwa na madhara kwenye mifumo ya afya kwa nchi za Pakistani na Afghanistan.”
 
Amegusia kuwa vikwazo vya aina mbalimbali vinaweza pia kukwamisha huduma za kitabibu dhidi ya Corona huko Cuba, Korea Kaskazini, Venezuela na Zimbabwe ambako amesema baadhi yao tayari mifumo ya afya ni dhaifu.
  
Amekumbusha kuwa ni muhimu kulinda afya za watoa huduma na kwamba madaktari hawapaswi kuadhibiwa kwa kubainisha udhaifu wanaokumbana nao wanapokabiliana na janga la Corona kwa kwa wao wako mstari wa mbele kumlinda kila mtu,
 
Bi. Bachelet ametoa wito kwa viongozi duniani kuwa kitu kimoja akisema mshikamano wa kimaitafa ni muhimu wakati wote katika kusongesha haki za binadamu na kwamba ni muhimu katika kusongesha maslahi ya kila taifa katika kipindi cha sasa.
 
COVID-19 imethibitishwa katika mataifa 189.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Grace Kaneiya
Audio Duration
2'7"
Photo Credit
UN Photo - Jean-Marc Ferre