Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwepo wa COVID-19 usitufanye tusahau kuhusu tishio la TB

Uwepo wa COVID-19 usitufanye tusahau kuhusu tishio la TB

Pakua

Tunapopambana na janga la kimataifa la afya COVID-19 ni wakati pia wa kutafakari na kutoyapa kisogo maradhi mengine makubwa ikiwemo kifua kikuu au TB, amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO. Flora Nducha na taarifa zaidi

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Mkurugenzi huyo Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus ameikumbusha dunia na kila mtu kwamba ingawa virusi vya corona, COVID-19 ndio vinavyogonjwa vichwa vya habari kila kona ya dunia kuna gonjwa lingine la mfumo wa hewa ambalo ni chagamoto kwa dunia

(SAUTI YA DKT. TEDROS CUT 1)
“Kuna ugonjwa mwingine wa mfumo wa hewa ambao unazuilika na kutibika lakini unakatili Maisha ya watu milioni 1.5 kila mwaka na gonjwa hilo la muda mrefu ni kifua kikuu.”

Ameongeza kuwa wakati dunia leo ikiadhimisha siku ya kifua kikuu duniani ambayo kila mwaka hua Machi 24, hii nifursa ya kuwakumbusha viongozi wa dunia kuhusu wajibu wao wa ahadi waliyoiweka ya kutokomeza madhila na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu mbaya na wa muda mrefu wa TB.

(SAUTI YA DKT. TEDROSS CUT 2)
“Dunia inachukua hatua muafaka na za haraka kukabiliana na COVID-19, tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukumbatia lengo na uharaka huo kwa vita dhidi ya kifua kikuu na kwa kuwa na dunia yenye afya, salama na ya usawa kwa kila mtu.”

Kaulimbiu ya siku ya mwaka huu ni “wakati umewadia kutokomeza TB” na tawkimu za WHO zinaonyesha kwamba kifua kikuu au TB ni ugonjwa wa kuambukiza unaokatili Maisha ya watu wengi zaidi duniani.

Kila siku zaidi ya watu 4000 wanakufa kutokana na TB na wengine zaidi ya 30,000 wanaugua ugonjwa huu ambao unazuilika na kutibika.

Na katika kuhakikisha gonjwa hili linatokomezwa WHO imetangaza muongozo mpya kuhusu matibabi ya kifua kikuu ambao utasaidia kuwa na matokeo mazuri ya tiba kwa wagonjwa kuokoa maisha.

Tangu mwaka 2000 Who inasema juhudi za kimataifa za kukabiliana na kifua kikuu zimeokoa Maisha ya watu milioni 58.

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Flora Nducha
Audio Duration
2'25"
Photo Credit
WHO