Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika miaka 65 ya umri wangu sijawahi kushuhudia amani-Rotto

Katika miaka 65 ya umri wangu sijawahi kushuhudia amani-Rotto

Pakua

Tangu nizaliwe sijawahi kushuhudia amani, hiyo ni kauli ya mkimbizi wa ndani wa Sudan Kusini John Rotto mwenye miaka 65, aliyezaliwa na kukulia kwenye vita. kulikoni? Jason Nyakundi anasimulia zaidi

(TAARIFA YA JASON NYAKUNDI)

Natts…

Katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Rimenze ndio maskani ya Rotto ambaye anatumai hataaga dunia akiishuhudia nchi yake bado iko vitani. Wakazi wa eneo hili walidhani kuna matumaini taifa lao lilipopata uhuru 2011,  Rotto akadhani ni wakati wa kupumzika na kupunga upepo ili kujenga upya maisha na mustakabali bora.

Lakini miaka miwili tu baada ya uhuru huo zahma ikazuka upya ikiwemo kijijini kwake Equatoria Magharibi ambako maelfu ya watu walikabiliwa na ukatili mkubwa ikiwemo wa kingono na kuwalazimisha kufungasha virago

(SAUTI YA ROTTO-1)
“Nyumba yangu ilichomwa moto mara mbili, mwaka wa kwanza nilikimbilia katika kambi hii na nikaikarabati utulivu uliporejea, kisha ikateketezwa tena, haya ndio madhila ninayoyapitia”

Kwa kuwa sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi na familia yake Rotto hawezi tena kupata kipato kutokana na kilimo na badala yake anategemea utengenezaji wa nyavu za kuvulia samaki ili kuishi, na kipato apatacho kwa siku ni takribani dola tatu na nusu

(SAUTI YA JOHN ROTTO-2)

“Hii ndio kazi ninayofanya ili kuweza kuishi kwa sababu haturuhusiwi kwenda nje ya kambi kulima”

Baada ya kuanzishwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa hivi karibuni Rotto na wenziwe wanaitaka amani kwa udi na uvumba

(SAUTI YA JOHN ROTTO-3)

“Bado tuna hofu, hatujaihisi amani ingawa tunaisikia, tunapaswa kuihisi huduma ya amani hii na ndipo itakuwa amani ya kweli.”

Watoto wa Rotto pia wamezaliwa vitani na anahofia mustakbali wao wasijepitia alichopitia

(SAUTI YA JOHN ROTTO -4)

“Hakuna amani, watoto wangu wawili wamezaliwa vitani.Sijui jinsi gani serikali itawasaidia watoto hawa kukua bila milio ya risasi. Vita vimeathiri akili zao na wamekuwa kama wendawazimu.”

Japo amekatishwa tamaa mara nyingi na miakataba ya amani inayovunjika safari hii anatumai kwamba fikra zake si sahihi na kwamba viongozi watawapa watoto wake usalama na mustakabali bora wanaostahili.

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Jason Nyakundi
Audio Duration
1'42"
Photo Credit
UNMISS\Nektarios Markogiannis