Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huko CAR mafuriko ya miezi minne iliyopita bado "mwiba" kwa wakazi

Huko CAR mafuriko ya miezi minne iliyopita bado "mwiba" kwa wakazi

Pakua

Miezi minne tangu mafuriko yaliyolazimisha takribani watu 28,000 kukimbia makazi yao kwenye mji wa Bangui, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR bado wakimbizi hao wa ndani wanakabiliwa na changamoto kubwa.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, kwenye mji mkuu Bangui, wakazi wanaonekana wakifua nguo kwenye mto Bangui.

Wengi wao wamekimbia makwao tangu mafuriko yapige maeneo yao mwaka jana.

Wanawake kwa watoto, upande mwingine ni hali ya mgeni njoo mwenyeji apone.

Ugeni wa wafanyakazi wa MINUSCA ni habari njema kwani wanatoa mgao kwa wakimbizi hao.

Carole Baudoin,ni mkuu wa kitengo cha mabadiliko na usalama kwenye MINUSCA ambaye anasema, "Kwetu sisi ni ishara ya umoja na ukarimu ambao wafanyakazi wa MINUSCA, timu ya kitaifa ilionesha. Waliamua kwenda kusaidia wahanga wa mafuriko ya mwishoni mwa mwaka 2019. leo nasi tukaamua tutoe mchango wetu kama wafanyakazi wa kimataifa, kuunga mkono juhudi za wafanyakazi wa kitaifa wa MINUSCA."

Wafanyakazi wa MINUSCA wamegawa nguo, viatu, chumvi, samaki wa makopo, sabuni na ndoo kwa wakimbizi hao. Christophe Kogbako mnufaika wa mgao huo anasema, "tunashukuru MINUSCA kwa msaada wao hapa leo. Awali tulikuwa tunaishi visiwa vya Gbongoussoua. Lakini kutokana na ongezeko la maji, nyumba zetu ziliharibika. Sasa hivi tunaishi katika kituo cha wakimbizi. Hakuna mtu ambaye anatusaidia. Kitu ambacho MINUSCA wamekifanya kimetufurahisha sana, tunafuraha sana."

Wengi wa wakazi walipoteza mali yao kufuatia mafuriko ya mwezi Oktoba mwaka jana yaliyosababishwa na mafuriko ya mito. Marie-Noëlle Gbolet ni moja wa wakimbizi ambaye hakuficha furaha yake akisema, "baada ya matatizo yote ambayo tumekuwa nayo, msaada huu unakaribishwa. Leo tutaweza kula na kushiba. Tunasema asante sana."

Wafanyakazi wa MINUSCA wameahidi kuendelea kusambaza bidhaa muhimu kwa watu waliofurushwa katika maeneo mengine ya Bangui na hususan walioathirika na mafuriko. 

 

 
Audio Credit
Grace Kaneiya
Audio Duration
2'21"
Photo Credit
MINUSCA