Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja baadaye, kimbunga Idai bado ni jinamizi kwa manusura wake

Mwaka mmoja baadaye, kimbunga Idai bado ni jinamizi kwa manusura wake

Pakua

Mwaka mmoja tangu kimbunga Idai kipige eneo la kati la Msumbiji idadi kubwa ya manusura ya janga hilo bado wameshindwa k urejea katika maisha ya kawaida kutokana na uhaba wa fedha za ukarabati. 

Kimbunga Idai kilipiga mji wa Beira katika jimbo la Sofala katikati mwa Msumbiji usiku wa Machi 14 na 15 ambapo kabla ya hapo kulishuhudiwa mvua kubwa na mafuriko katika nchi tatu ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kusababisha maelfu ya watu kufurushwa makwao na vifo na uharibifu wa mali.

Wiki zilizofuatia zahma hizi zilishuhudia shirika la mpango wa chakula duniani, WFP likianza kusambaza misaada kwa watu milioni 1.8, hata hivyo wengi wao hadi leo hii bado wanahaha, bila kufahamu mustakabali wao.

Miongoni mwao ni Elisa mama wa watoto watatu“Nyumba yetu ilipoanza kubomoka, mimi na watoto tulikimbilia shule kujikinga na mvua. Nyumba nyingi zilibomoka na hatukuweza kuokoa chochote, kila kitu kiliharibika.”

WFP ilianzisha mradi wa kupatia chakula manusura, FFA lakini kwa kufanya kazi kwenye miradi kama vile mashamba ya kijamii na ujenzi wa madaraja katika wilaya ya Nhamanda jimboni Sofala.

Wakulima hawa wanapanda mihogo, mpunga, mananasi na kisha wanauza bidhaa zao ili wanunue mbegu kwa mazao mengine. Hata hivyo mwezi uliopita, ukata ulisababisha WFP ikate kwa asilimia 50 mgao wake kwa wakazi  525,000 wanaofanya kazi kwenye miradi hii.

Pamoja na miradi hiyo, WFP inawapatia vocha ya dola 40 kila mwezi ili waweze kununua bidhaa watakazo ikiwemo chakula. WFP inasema kwa mwaka huu wa 2020 inahitaji dola milioni 991 ili iweze kutekeleza kwa kina miradi yake ya ukarabati kwa ajili ya manusura wa kimbunga Idai.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'3"
Photo Credit
UNHCR/Zinyange Auntony