Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

12 Machi 2020

12 Machi 2020

Pakua

FLORA: Hujambo na Karibu kusikiliza Jarida kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kutoka hapa New York Marekani.

JINGLE (04”)     

FLORA: Ni Alhamisi ya Machi 12 mwaka 2020, mwenyeji wako studioni hii leo ni mimi FLORA NDUCHA

1: Kimbunga Idai bado ni jinamizi kwa manusura wake

Mwaka mmoja tangu kimbunga Idai kipige eneo la kati la Msumbiji idadi kubwa ya manusura ya janga hilo bado wameshindwa kurejea katika maisha ya kawaida kutokana na uhaba wa fedha za ukarabati huku shirika la mpango wa chakula duniani, WFP ikisema inahitaji dola milioni 991 kwa mwaka huu wa 2020 ili kunusuru watu hao. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Nats…

Kimbunga Idai kilipiga mji wa Beira katika jimbo la Sofala katikati mwa Msumbiji usiku wa Machi 14 na 15 ambapo kabla ya hapo kulishuhudiwa mvua kubwa na mafuriko katika nchi tatu ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kusababisha maelfu ya watu kufurushwa makwao na vifo na uharibifu wa mali.

Wiki zilizofuatia zahma hizi zilishuhudia shirika la mpango wa chakula duniani, WFP likianza kusambaza misaada kwa watu milioni 1.8, hata hivyo wengi wao hadi leo hii bado wanahaha, bila kufahamu mustakabali wao.

Miongoni mwao ni Elisa mama wa watoto watatu

(Sauti ya Elisa)

“Nyumba yetu ilipoanza kubomoka, mimi na watoto tulikimbilia shule kujikinga na mvua. Nyumba nyingi zilibomoka na hatukuweza kuokoa chochote, kila kitu kiliharibika.”

WFP ilianzisha mradi wa kupatia chakula manusura, FFA lakini kwa kufanya kazi kwenye miradi kama vile mashamba ya kijamii na ujenzi wa madaraja katika wilaya ya Nhamanda jimboni Sofala.

Wakulima hawa wanapanda mihogo, mpunga, mananasi na kisha wanauza bidhaa zao ili wanunue mbegu kwa mazao mengine.

Hata hivyo mwezi uliopita, ukata ulisababisha WFP ikate kwa asilimia 50 mgao wake kwa wakazi  525,000 wanaofanya kazi kwenye miradi hii.

Pamoja na miradi hiyo, WFP inawapatia vocha ya dola 40 kila mwezi ili waweze kununua bidhaa watakazo ikiwemo chakula.

WFP inasema kwa mwaka huu wa 2020 inahitaji dola milioni 991 ili iweze kutekeleza kwa kina miradi yake ya ukarabati kwa ajili ya manusura wa kimbunga Idai.

===================================================

2: Ukarimu wa wafanyakazi wa MINUSCA waleta faraja kwa waathirika wa mafuriko CAR

Miezi minne tangu mafuriko yaliyolazimisha takribani watu 28,000 kukimbia makazi yao kwenye mji wa Bangui, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR bado wakimbizi hao wa ndani wanakabiliwa na changamoto kubwa.Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Nats..

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, kwenye mji mkuu Bangui, wakazi wanaonekana wakifua nguo kwenye mto Bangui.

Wengi wao wamekimbia  makwao tangu mafuriko yapige maeneo yao mwaka jana.

Wanawake kwa watoto, upande mwingine ni hali ya mgeni njoo mwenyeji apone.

Ugeni wa wafanyakazi wa MINUSCA ni habari njema kwani wanatoa mgao kwa wakimbizi hao.

Carole Baudoin,ni mkuu wa kitengo cha mabadiliko na usalama kwenye MINUSCA kulikoni,

(Sauti ya Carole)

“Kwetu sisi ni ishara ya umoja na ukarimu ambao wafanyakazi wa MINUSCA, timu ya kitaifa ilionesha. Waliamua kwenda kusaidia wahanga wa mafuriko ya mwishoni mwa mwaka 2019. leo nasi tukaamua tutoe mchango wetu kama wafanyakazi wa kimataifa, kuunga mkono juhudi za wafanyakazi wa kitaifa wa MINUSCA.”

Wafanyakazi wa MINUSCA wamegawa nguo, viatu, chumvi, samaki wa makopo, sabuni na ndoo kwa wakimbizi hao. Christophe Kogbako mnufaika wa mgao huo  anasema

(Sauti ya Christophe)

“Tunashukuru MINUSCA kwa msaada wao hapa leo. Awali tulikuwa tunaishi visiwa vya Gbongoussoua [BONGUSWA]. Lakini kutokana na ongezeko la maji, nyumba zetu ziliharibika. Sasa hivi tunaishi katika kituo cha wakimbizi. Hakuna mtu ambaye anatusaidia. Kitu ambacho MINUSCA wamekifanya kimetufurahisha sana, tunafuraha sana.”

Wengi wa wakazi walipoteza mali yao kufuatia mafuriko ya mwezi Oktoba mwaka jana yaliyosababishwa na mafuriko ya mito. Marie-Noëlle Gbolet ni moja wa wakimbizi

(Sauti ya Marie)

“Baada ya matatizo yote ambayo tumekuwa nayo, msaada huu unakaribishwa. Leo tutaweza kula na kushiba. Tunasema asante sana.”

Wafanyakazi wa MINUSCA wameahidi kuendelea kusambaza bidhaa muhimu kwa watu waliofurushwa katika maeneo mengine ya Bangui na hususan walioathirika na mafuriko. 

====================================================

STUDIO. MIDWAYSTING

====================================================

FLORA : Na punde ni Mashinani ambapo tutakuwa jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini, usibanduke!

====================================================

3: Siku zote baada ya dhiki ni faraja:Mkimbizi Ould

Kutana na Sidi Ould Amin, raia wa Mali aliyekimbia nchi yake hiyo hadi Burkina Faso, lakini sasa  amerejea nyumbani na kuanzisha biashara ya ufundi cherahani, kwa kutumia ujuzi alioupata kupitia mafunzo ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR akiwa kwenye kambi ya wakimbizi nchini Mali.  Jason Nyakundi na tarifa zaidi

(TAARIFA YA JASON NYAKUNDI)

NATS…..Mjini Mpoti Mali Sid Ould Amin mwenye umri wa miaka 37 akiwa nyumbani kwake na familia yake baada ya kurejea kutoka ukimbizi nchini Burkina Faso alikokimbilia mwaka 2012 baada ya vita kuzuka nchini Mali na kupoteza kila kitu

(SAUTI YA OULD AMIN-1)

« Tukawa masikini wa kutupa, kabla ya vita tulikuwa vizuri, lakini baada ya zahma hii, uharibifu, wizi, na mashambulizi hatua chochote kilichosalia. »Tangu mwaka 2012 zaidi ya watu 130,000 wamefungasha virago Mali na kukimbia vita.

(SAUTI YA OULD AMIN-2)

« Sikutaka kuondoka lakini unapolazimika inabidi uondoke.Ukiona kinachoendelea basi huna budi kuondoka »

Kwenye kambi ya wakimbizi alikokimbilia Burkina Faso Ould alipatiwa msaada, ulinzi na hata mafunzo yanayotolewa na UNHCR ikiwemo utengenezaji wa sabuni, ufundi makenika na ufundi cherahani

(SAUTI YA OULD AMIN-3 )

« Nilipoambiwa kwamba mafunzo ya ufundi cherahani yapo, nikasema hayo ndio ninayoyapendelea kufanya kwa sababu nguo za watoto wangu nyumbani zimechanika »

Mwaka 2017 Ould aliamua kurejea nyumbani Mali na kufungua biashara ya ufundi cherahani, kwake ametimiza ndoto kwani baada ya dhiki ni faraja na sasa anatoa shukran kwa jamii yake kwa kuwafundisha vijana wasichana kwa wavulana ambao ni watoto wa mitaani mafunzo ya ushonaji ili waachane ta hulka ya kuombaomba mitaani

===================================================

STUDIO: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under

====================================================

FLORA:  Na sasa ni makala ambapo nampisha Assumpta Massoi katika mahojiano ya awali na Katibu Mkuu wa Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi akizunugmzia mazingira ya sasa ya kisiasa na changamoto zingine zinazokwamisha ufadhili wa SDGs

=================================================

STUDIO: PLAY MAKALA

====================================================

 

FLORA: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under

====================================================

FLORA:  Shukran Assumpta Massoi na Dkt. Mukhisa Kituyi kwa makala hiyo.

====================================================

Na sasa ni mashinani ambapo Christopher Muchiri Murenga, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ofisi ya mjini Yambio, Equatoria Magharibi anatoa ahadi ya kuendelea kuwaunga mkono wanawake wa Sudan Kusini walipokusanyika kusherehekea utamaduni wao pamoja na siku ya wanawake duniani.

 

====================================================

Studio: Play Mashinani

====================================================

FLORA: Shukrani sana Christopher Muchiri kutoka Sudan Kusini, mjini Yambio.

==================================================

STUDIO: Play Bridge

FLORA: Na hadi hapo natamatisha jarida letu la leo. Hadi wakati mwingine kwa habari na makala kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa unaweza kupata matangazo na taarifa nyingine na kujifunza Kiswahili kwenye wavuti wetu news.un.org/sw. Msimamizi  wa matangazo ni GRACE KANEYA na fundi mitambo ni Carlos Macias na mimi FLORA NDUCHA, nasema kwaheri kutoka New York.

 

==================================================

TAPE: CLOSING BAND

Audio Credit
Flora nducha
Audio Duration
12'5"