Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti mpya yaonesha kuna ongezeko la ishara na madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika anga, ardhi na baharini

Ripoti mpya yaonesha kuna ongezeko la ishara na madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika anga, ardhi na baharini

Pakua

Ishara za mabadiliko ya tabianchi kama vile ongezeko la joto la ardhini na baharini, kuongezeka kwa kina cha bahari na kuyeyuka kwa barafu, vimeangaziwa katika ripoti mpya ya Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO na wadau wake iliyotolewa hii leo Machi 10 mjini New York Marekani na Geneva Uswisi. 

Ripoti hiyo imeeleza madhara ya matukio ya hali ya hewa na tabianchi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, afya ya binadamu, uhamiaji na ukosefu wa makazi, uhakika wa chakula, ardhi na maisha ya viumbe vya majini.

Taarifa hiyo ya WMO kuhusu hali ya tabianchi ya ulimwengu kwa mwaka 2019 inajumuisha mchango wa taaarifa kutoka mamlaka za hali ya hewa na maji za mataifa mbalimbali, wataalamu wa kimataifa, taasisi za sayansi na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

 Ripoti hiyo inatoa taarifa muhimu kwa watunga sera kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti hii inathibitisha taarifa iliyotolewa awali wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mwezi Desemba mwaka jana kuwa mwaka huo wa 2019 ulikuwa wa pili kwa kuwa na joto la juu katika rekodi ambapo mwaka 2015 hadi 2019 ni miaka mitano iliyokuwa na joto zaidi katika rekodi za joto huku mwaka 2010 hadi 2019 ni muongo uliorekodiwa kuwa na joto la juu.

 Tangu mwaka 1980, kila muongo umekuwa na joto la juu zaidi ya muongo uliotangulia tofauti na ilivyokuwa kwa miongo mingine ya kuanzia mwaka 1850.

Mwaka 2019 ulikamilika na wastani wa joto la dunia la nyuzi joto 1.1°C juu ya makadirio ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, rekodi ya pili baada ya ile ya mwaka 2016 wakati ambapo tukio la El Nino lilichangia katika ongezeko la joto juu ya mwenendo wa Jumla wa ongezeko la joto.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumzia taarifa hiyo kupitia dibaji ya ripoti hiyo amenukuliwa akisema, “kwa sasa tuko nyuma ya muda katika mbio za ama kufikia lengo la nyuzi joto 1.5 au 2 ambazo Mkataba wa Paris unatolea wito.”

Naye Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema, “kwa kuwa viwango vya hewa chafuzi  vinaongezeka, ongezeko la joto litaaendelea. Utabiri wa hivi karibuni unaonesha kuwa rekodi mpya ya mwaka ya dunia inaweza kutokea katika miaka mitano ijayo. Ni suala la muda.”

 

Audio Credit
Jason Nyakundi
Sauti
2'29"
Photo Credit
WMO/Vladimir Tadic