Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa Javier Pérez  de Cuéllar amefariki dunia

Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa Javier Pérez  de Cuéllar amefariki dunia

Pakua

Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa Javier Pérez  de Cuéllar amefariki dunia. Alikuwa na umri wa miaka 100. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

De Cuéllar raia wa Peru ambaye amefariku dunia Jumatano ya Machi 03, alihudumu mihula miwili kwenye Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe  Januari mwaka 1982 hadi tarehe 31 Desemba mwaka 1991.

Kufuatia taarifa za kifo chake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa taarifa kupitia msemaji wake akieleza masikitiko  yake makubwa kufuatia kifo cha de Cuéllar.

 Amemwelezea kuwa mwanasiasa mzoefu, mwenye stadi na mwanadiplomasia aliyejizatiti na mtu ambaye aliacha alama kubwa kwenye Umoja wa Mataifa na duniani kote.

Ameenda mbali akisema kuwa maisha ya Pérez de Cuéllar yamekuwa ya siyo tu karne moja bali pia historia nzima ya Umoja wa Mataifa kuanzia ushiriki wake katika mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1946.

Guterres amesema kipindi chake cha  uongozi akiwa Katibu Mkuu kiliendana na zama mbili muhimu ambazo ni mosi, “baadhi ya miaka migumu ya vita baridi na hatimaye mzozano wa kiitikadi kipindi ambacho Umoja wa Mataifa ulianza kutekeleza kwa dhati dhima iliyobuniwa na waasisi wa umoja huo.”

Pérez de Cuéllar alikuwa na dhima muhimu katika maeneo muhimu yaliyokuwa ni mafaniki kidiplomasia ikiwemo uhuru wa Namibia, kumalizika kwa vita kati ya Iraq na Iran, kuachiliwa huru kwa mateka wa kimarekani waliokuwa wakishikiliwa nchini Lebanon, mkataba wa amani nchini Cambodia na katika siku zake za mwisho kabisa ofisini mkataba wa amani wa kihistoria nchini El Salvador.

Katibu Mkuu ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Pérez de Cuéllar, wananchi wa Peru na watu wengine wengi duniani kote ambao maisha yao yaliguswa na kiongozi huyo wa kimataifa ambaye ameaga dunia na kuiacha pahala bora zaidi.

Wakati huo huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Ban  Ki Moon ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha De Cuellar akisema kuwa akiwa ni mtangulizi wake, busara, muongozo na hamasa vilimsaidia Ban wakati wa kipindi chake kuanzia mwaka 2007 hadi 2016.

Akiondoka madarakani kama Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa katika majira ya kiangazi mwaka 1991 de Cuéllar alitoa ripoti yake ya mwisho ambayo ilikuwa tofauti na ya kwanza safari hii aliandika about kufufua Umoja wa Mataifa, kumaliza mkwamo wa muda mrefu.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'12"
Photo Credit
UN Photo/John Isaac