Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa mjadala kuhusu katiba unalenga kuhakikisha ujumuishwaji wa sauti za raia Somalia

Mkutano wa mjadala kuhusu katiba unalenga kuhakikisha ujumuishwaji wa sauti za raia Somalia

Pakua

Zaidi ya watu 100 huko Baidoa jimbo la Kusini-Magharibi nchini Somalia, wameshiriki mkutano wa majadiliano ya sehemu ya mchakato wa katiba inayolenga kuchukua nafasi ya katiba ya muda iliyopitishwa mwaka 2012 kabla ya uchaguzi wa mtu mmoja kura moja mwaka huu wa 2020. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Washiriki wa mkutano huo ulioratibiwa na Wizara ya masuala ya katiba na pia kwa msaada wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, ni pamoja na wawakilishi wa jamii wakiwemo wakuu wa kaya, vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na viongozi wa kidini.

Wamebadilishana mawazo kuhusu mamlaka na ugawaji wa rasilimali, uongozi, uchaguzi, mfumo wa mahakama na usalama wa kitaifa.

Salima Sheikh Shueb, mwakilishi wa kundi la wanawake ameomba uwakilishi wa wanawake katika nafasi za kuchaguliwa na kwenye huduma ya umma.

(Sauti ya Salima)

“Katiba inahitaji kuyapa kipaumbele masuala ya wanawake. Ijapokuwa inasemwa kuwa wanawake wanapaswa kuwa na asilimia 30 ya uwakilishi, hiyo haitoshi. Ni lazima tupate asilimia 50. Uwakilishi wetu haupaswi tu kuwa kwenye serikali au bunge lakini ni lazima tuwakilishwe kila mahali, ikiwemo kwenye wizara na taasisi zingine kwenye serikali.”

Kwa upande wake Mukhtar Ali Isak akiwakilisha watu wenye ulemwavu amesema katiba inahitaji kuhakikisha kwamba haki za kundi hilo ushiriki wao kwenye maendeleo ya kitaifa.

(Sauti ya Mukhtar)

“Tunataka watu wenye ulemavu wawe na fursa ya kushiriki katika siasa, na uwakilishi katika vyama vya siasa, baraza mashinani, bunge, kamati huru na taasisi zingine. Hilo ndio ombi letu kwa serikali kuu na seriklai ya jimbo tunakoishi.”

Naye kamishna wa wilaya ya Baidoa, Hassan Moalim Ahmed Bikole amewahimiza watu kushiriki na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya majadiliano ya wazi kufikia kufanikisha katiba.

(Sauti ya Hassan)

“Maoni yenu ni muhimu, iwapo hautashirika na kutaja yale mazuri na mabaya kwenu sisi, hautakuwa unatekeleza wajibu wako kama raia. Hii ndio fursa yako kushiriki katika kampeni hii ya kitaifa na kurekebisha makosa unayoyaona ili usihisi kama umetengwa.”

Mkutano huu ni wa pili katika kampeni ya kitaifa inayolenga majimbo yote ya Somalia kwa ajili ya kuwezesha raia kuchangia katika mchakato wa kuunda katiba.

Audio Credit
UN News/Grace Kaneiya
Sauti
2'25"
Photo Credit
UN Photo/Ilyas Ahmed)