Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasema dola milioni 59.4 zahitaji kunusuru watoto Niger 2020

UNICEF yasema dola milioni 59.4 zahitaji kunusuru watoto Niger 2020

Pakua

Nchini Niger, takribani watu milioni 3 wanahitaji, zaidi ya nusu yao wakiwa ni watoto,wanahitaji msaada wa kibinadamu wakati huu ambapo taifa hilo linakabiliwa na ukosefu wa usalama, utapiamlo, magonjwa, mafuriko na ukimbizi wa ndani. Brenda Mbaitsa na maelezo zaidi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hayo leo kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Diffa, nchini Niger, ikitoa wito kwa hatua zaidi ili kusaidia watoto na familia zao kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi.

UNICEF inasema Niger inaendelea kukumbwa na dharura  kila uchao na hivyo kusababisha wadau wa kibinadamu kushindwa kuchukua hatua zipasazo za usaidizi kwa wanawake na watoto na kwamba hali hiyo inachochewa zaidi na ukosefu wa utulivu kwenye ukanda huo ikiwemo nchi jirani.

“Wakimbizi wanazidi kumiminika nchini Niger na wao na wenyeji wao wanahitaji huduma za msingi za kijamii pamoja na ulinzi,”  amesema Dkt. Félicité Tchibindat ambaye ametembelea eneo la Diffa akiwa ameambatana na wadau wa kimataifa na marafiki wa Niger.

Amesema kuwa wenyeji wanaowasaidia wakimbizi wameonyesha ukarimu wa kupindukia kwa kugawana na wageni wao kidogo walicho nacho bila tafrani yoyote na kwamba huo ni mfano mkubwa ambao wananchi wa Niger wanaonyesha kwa ulimwengu mzima.

Dkt. Tchibindat amesema kadri msisitizo zaidi wa usaidizi unavyoelekezwa ukanda wa kati wa Sahel, vivyo  hivyo msisitizo huo uelekezwe kwenye athari wanazopata watoto na familia zao.

Mathalani amesema  ukosefu wa usalama  tayari umeongeza changamoto wanazopata watoto, kwa kuwa ukimbizi unaathiri afya, ulinzi, lishe na elimu kwa watoto.

Ukosefu wa usalama pia amesema unasababisha wahudumu wa kibinadamu washindwe kufikia jamii zilizoathiriwa na mzozo na hivyo UNICEF inatoa wito kwa wadau wote kuheshimu maeneo ya kibinadamu ili waathiriwa wakiwemo wanawake na watoto waweze kufikishiwa misaada.

Nchini Niger, UNICEF inashughulikia vipaumbele ili iweze kufikia haraka wananchi wenye mahitaji na kwamba imesema yenyewe na wadau wake watahitaji dola milioni 59.4 ili kuweza kufikisha mahitaji muhimu kwa watoto kwa mwaka huu wa 2020.

Audio Credit
UN News/Brenda Mbaitsa
Audio Duration
2'15"
Photo Credit
© UNICEF/Vincent Tremeau