Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN ashiriki utoaji chanjo dhidi ya Polio Pakistani

Katibu Mkuu wa UN ashiriki utoaji chanjo dhidi ya Polio Pakistani

Pakua

Hii leo akiendelea na ziara yake nchini Pakistani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshiriki katika kampeni  ya utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwenye mji wa Lahore. Taarifa kamili na Brenda Mbaitsa

Kampeni hiyo ya kwanza ya kitaifa ya mwaka inayofanyika mwezi huu wa Februari inalenga kufikia zaidi ya watoto milioni 39 nchini humo katika taifa hilo ambamo mwaka jana pekee kulikuwepo na ongezeko kubwa la visa vya polio na polio pori mwaka jana na mwaka huu pekee tayari kuna wagonjwa 17.

Katika tukio hilo Bwana Guterres alipatia matone ya chanjo wanafunzi watatu, na kisha kupongeza Pakistani kwa harakati zake za kutokomeza ugonjwa huo akiongeza kuwa polio ni ugonjwa ambao jamii ya kimataifa inaweza kutokomeza katika miaka michache ijayo.

Amesema azma hiyo ni kipaumbele cha Umoja wa Mataifa na amefurahi sana kuona kuwa ni kipaumbele dhahiri pia cha serikali ya Pakistani.

Hata hivyo ametoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wa kidini na kijamii kuunga mkono kwa dhati serikali  ya Pakistani na serikali nyingine zote duniani kuhakikisha kuwa dunia inaweza kutokomeza ugonjwa wa polio.

Wakati wa ziara hiyo Katibu Mkuu amekutana na wahudumu wa afya walio mstari wa mbele wakitoa chanjo dhidi ya polio na kuelezea mshikamano wake na wahudumu hao ambao sasa idadi yao ni 265,000.

Wahudumu hao wanatembea kaya kwa kaya kuhakikisha kuwa watoto wengi zaidi wanapatiwa chanjo dhidi ya polio na ambapo asilimia 62 ya wafanyakazi hao ni wanawake.

Audio Credit
UN News/Brenda Mbaitsa
Audio Duration
1'29"
Photo Credit
UN News/May Yaacoub