Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 58 wafa maji kando mwa pwani ya Mauritania wakielekea Ulaya

Watu 58 wafa maji kando mwa pwani ya Mauritania wakielekea Ulaya

Pakua

Takribani watu 58 wamethibitishwa kufa maji baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama wakati ikikaribia pwani  ya Mauritania hii leo. Anold Kayanda na maelezo zaidi.

Taarifa ya shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM iliyotolewa mjini Nouadhibou hii leo imesema kuwa manusura 83 wanapatiwa msaada kutoka mamlaka za Mauritania, IOM pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Manusura hao wamewaeleza wafanyakazi wa IOM huko Nouadhibou, mji wa pili kwa ukubwa nchini Mauritania kuwa takribani watu 150 wakiwemo wanawake na watoto walikuwa kwenye boti hiyo ambayo ilianza safari yake tarehe 11 ya mwezi uliopita huko Gambia.

Wamesema kuwa boti hiyo ilikuwa inaishiwa mafuta pind ilipokaribia taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Mkuu wa IOM nchini Mauritania Laura Lungarotti amepongeza mamlaka za taifa hilo kwa ufanisi wake katika kushughulikia janga hilo kwa ushirikiano na IOM na UNHCR akisema kuwa, “kipaumbele chetu cha pamoja ni kuwahudumia manusura na kuwapatia msaada wanaohitaji.”

IOM inasema majeruhi wamehamishiwa katika hospitali ya jiji hilo na kwamba inapeleka daktari kusaidia wahudumu wengine kwenye hospitali hiyo.

Hivi sasa mamlaka za Mauritania zinawasiliana na zile za vibali za Gambia ili kuhakikisha zinapata msaada  unaohitajika kwa wahamiaji hao huku balozi wa Gambia akielekea mjini humo.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Anold Kayanda
Audio Duration
1'26"
Photo Credit
UNHCR/Federico Scoppa