Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa vichomi waendelea kutesa watoto, Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyo ya idadi ya juu ya vifo- WHO

Ugonjwa wa vichomi waendelea kutesa watoto, Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyo ya idadi ya juu ya vifo- WHO

Pakua

Ugonjwa unaozuilika wa kichomi unakatili maisha ya watoto  wengi kuliko maradhi mengine yoyote kwa mujibu wa taarifa ya utafiti mpya iliyotolewa leo na mashirika matano ya kimataifa yanayohusika na masuala ya watoto likiwemo la Umoja wa Mataifa la UNICEF.  Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na UNICEF, ubia wa chanjo duniani GAVI, Save the children, Every Breath Counts na Unitaid,  kwa mwaka jana pekee ugonjwa wa kichomi ulikatili maisha ya watoto zaidi ya laki 8 walio na umri wa chini ya miaka mitano sawa na mtoto 1 kila sekunde 39.

Utafiti huo umesema vifo vingi hutokea kwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili na takribani vifoo 153,000 hutokea ndani ya mwezi mmoja wa maisha yao.

Ili kutoa tahadhari ya ugonjwa huo uliosahaulika mashirika hayo matano leo yamezindua wito wa kimataifa wa kuchukua hatua ambao utafuatiwa na kongamano la kimataifa la ugonjwa wa kichomi utotoni litakalofanyika nchini Hispania mwezi Januari mwakani.

Akisisitiza kuhusu ukubwa wa tatizo hilo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema “Kila siku karibu watoto 2,200 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki duniani kutokana na kichomi ugonjwa unaotibika na kuzuilika, hivyo hatua imara za kimataifa na kuongeza uwekezaji ni muhimu kukabiliana na ugonjwa huu. Ni kwa kupitia miradi ya gharama nafuu, kinga na matibabu kufikishwa waliko watoto walioathirika ndipo tutaweza kuokoa maisha ya mamilioni ‘’

Kichomi ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria , virusi au fangasi na hufanya watoto kupata matatizo ya kupumua kutokana na mapafu yao kujaa usaha na maji.

Kwa mwaka 2018 utafiti huo unasema watoto wengi zaidi wa chini ya umri wa miaka 5 walikufa kwa  kichomi kuliko ugonjwa mwingine wowote, mwaka ambao ulishuhudia vifo vya watoto kutokana na ugonjwa kwa kuhara   437,000 walio chini ya umri wa miaka 5 na vifo 272,000 vilivotokana na malaria kwa watoto wa umri huohuo.

Na nchi tano ndizo zilizohusika na idadi zaidi ya nusu ya vifo vyote vya kichomi duniani kwa mwaka jana ambazo ni Nigeria (162,000), India (127,000), Pakistan (58,000) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC (40,000) na Ethiopia (32,000). Nchi nyingine zilizoathirika na ugonjwa huu ni Indonesia (19,000), China (18,000) , Chad (18,000), Angola( 16,000) na Tanzania (15,000)

 

Audio Credit
Flora Nducha/Grace Kaneiya
Sauti
2'15"
Photo Credit
© UNICEF/Sebastian Rich