Nchi za Afrika zifanye biashara baina yao ili AfCFTA iwe na mashiko zaidi- Trademark East Africa

6 Novemba 2019

Mkutano wa 23 wa kamati ya watendaji wa serikali na wataalamu unaoangazia jinsi ya kusaka fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara wa kikanda kwenye eneo la mashariki mwa Afrika ukiingia siku ya pili hii leo huko Asmara, Eritrea, kampuni  ya Trademark East Africa imezungumzia kile ambacho nchi za Afrika zinapaswa kuzingatia ili kunufaika na eneo la soko huru barani humo, AfCFTA.

Mkurugenzi wa Utafiti wa kampuni hiyo Dkt. Anthony Mveyange akihojiwa na  Priscilla Lecomte wa Umoja wa Mataifa kandoni mwa mkutano huo amesema kuwa, "eneo ambalo AcFTA limeonekana kuwa ina nafasi nzuri na chachu ya kuleta maendeleo katika ukanda huu ni kuboresha uwezo wa nchi kuzalisha bidhaa.  Afrika inabidi ifanye biashara na Afrika  tuache kutegemea  zaidi kutoka nje. AFrika ina watu takribani bilioni 1.2. Watu bilioni 1.2 ni wengi. Sasa tunawezaje kuboresha uwezo wa watu kuzalisha ndani ya Afrika. Ni  namna gani tunaweza kuboresha mikakati madhubuti  ya kuwezesha nchi kufanya biashara  baina yetu."

Dkt. Mveyange, pamoja na kutaja mambo hayo amekumbusha kuwa AcFTA pekee si suluhu bali biashara kati ya nchi za Afrika, hivyo kile ambacho TradeMark wanafanya ni kusaka mbinu "ni namna gani itakuwa rahisi kwa mfano kutoka Ethiopia kufanya biashara na Kenya,  badala ya Ethiopia kuagiza bidhaa kutoka China au India,  ni namna gani Ethiopia na Kenya zinaweza kufanya biashara kwa urahisi zaidi, namna gani Kenya na Malawi zinaweza kufanya biashara kwa urahisi zaidi. Hiyo ni aina mojawapo, aina ya pili ni namna gani kujengea uwezo asasi za kibiashara Afrika zinaweza kujengewa uwezo na kuzipa nafasi kama masoko na teknolojia ya kuweza kuzalisha na ndivyo ambavyo kwa namna moja au nyingine tunaweza kuongeza ajira. Kwa sababu ili kuongeza ajira lazima tujenge uwezo iwe kwa minyororo ya thamani au kuongeza uzalishaji wa ndani bila kutegemea nje."

TradeMark ambayo inashirikiana na Umoja wa Mataifa kupitia Tume ya Uchumi ya umoja huo kwa nchi za Africa, UNECA na hufanya  tafiti pamoja kwa lengo la kuona AcFTA inabadilika kutoka nadharia kuwa vitendo.

Hivi sasa inaendesha shughuli zake Kenya, Zambia, Malawi, Tanzania,Uganda, Rwanda, Ethiopia  na wanaelekea Somaliland.

 

Audio Credit:
Assumpta Massoi
Audio Duration:
2'28"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud