Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni dhidi ya kipindupindu yaimarishwa huko Khartoum nchini Sudan

Kampeni dhidi ya kipindupindu yaimarishwa huko Khartoum nchini Sudan

Pakua

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, linashirikiana na wadau wake kusaidia kuepusha kuenea zaidi kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye jimbo la Khartoum nchini Sudan ikiwemo mji mkuu Khartoum. Brenda Mbaitsa na ripoti kamili.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Dkt. Naeema Al Gasseer amenukuliwa katika taarifa iliyotolewa leo mjini Khartoum akisema kuwa hatua ya shirika hilo inafuatia ombi la Waziri wa Afya wa Sudan Dkt. Akram Eltoum.

Dkt. Al Gasseer amesema kinachofanyika sasa ni kuhakikisha kuwa watu wote wanaoshukiwa kuugua Kipindupindu wanatambuliwa na kupatiwa matibabu haraka, na watu wengine waweze kujikinga na ugonjwa huo.

Tayari Wizara ya Afya na WHO wamebainisha maeneo  yaliyo hatarini zaidi kupata kipindupindu kwenye jimbo la Khartoum na hatua hiyo itasaidia kuweka mipango bora zaidi ya kudhibiti mlipuko kwenye maeneo hayo ikiwemo vitongoji vya Sharq Elnil na Ombada.

Na ili kuhakikisha kuwa vituo vya afya na vile vya kutibu kipindupindu vina vifaa vya kutosha kubaini na kutibu wagonjwa, WHO imesambaza dawa za tiba zinazoweza kutosha wagonjwa 400 na vipimo 500 vya kubaini haraka kipindupindu.

Halikadhalika wanasaidia kuanzisha vituo viwili vya kutibu kipindupindu kwenye vitongoji vya Ombada na Bahri na kuvipatia pia dawa za tiba, vifaa vya matibabu na vya kupima na wanapatia mafunzo wahudumu wa afya 271.

Dkt. Al Gasseer amekumbusha kuwa msingi wa kudhibiti kuenea kwa kipindupindu ni jinsi gani jamii inaweza yenyewe kujikinga, kwa hiyo wanashirikiana na waelimishaji wa afya 1700 wa kike na wa kiume na wafanyakazi wa kujitolea kuelimisha jamii juu ya kujikinga na kipindupindu.

WHO inasema hatari ya kusambaa kwa kipindupindu ni kubwa mno na iwapo hatua sahihi hazitachukuliwa, madhara makubwa yanaweza kutokea kwa kuzingatia kuwa zaidi ya watu milioni 8 wanaishi jimbo la Khartoum, ambako janga la uchumi na mafuriko ya hivi karibuni vimesambaratisha mifumo ya afya ya umma.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Brenda Mbaitsa
Audio Duration
2'15"
Photo Credit
© UNICEF