Matangazo ya shule kwa njia ya redio kusaidia watoto waliokimbia shule kutokana na ghasia Cameroon- UNICEF

5 Novemba 2019

Miaka mitatu ya ghasia na vurugu maeneo ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Cameroon zimefanya zaidi ya watoto 855,000 washindwe kwenda  shuleni, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF . Brenda Mbaitsa na ripoti kamili.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo New York, Marekani, Dakar, Senegal na Geneva Uswisi imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Henrietta Fore akisema kuwa bila ya hatua za dharura na kujitolea kutoka pande zote katika mzozo huo katika kulinda elimu kwa njia zote, hatma ya watoto hao iko hatarini.

Amesema maelfu ya watoto nchini Cameroon wanaishi kwa hofu na wanataka amani ili wapate kerejelea elimu yao kwa maisha yao ya baadaye.

UNICEF insema miezi miwili tangu kuanza kwa mwaka mpya wa shule, karibu asilimia 90 ya shule za msingi za umma ikiwa ni zaidi ya shule 4,100 na asilimia 77 ya sekondari za umma au shule 774 zimebaki zimefungwa katika meneo ya Kaskazini magharibi na kusini magharibi. 

Hofu ya kuzuka ghasia imesababisha wazazi wengi kutowapeleka watoto wao shuleni na walimu kutofika kazini.

Kati ya watoto hao, takribani watoto Laki Moja na Nusu wamehama makwao hali inayosababisha kuwaongezea mihangaiko.

Katika sehemu nyingine, shule zimefungwa na UNICEF inagawa vitabu na vifaa vingine vya masomo kwa watoto elfu 37, kuwasaidia katika masomo yao.

Halikadhalika, UNICEF itaandaa vipindi vya masomo kwa njia ya radio kwa watoto wanaobaki nyumbani.

Masomo hayo yamerekodiwa kwa msaada ya UNICEF na yatawsaidia watoto katika somo la hesabu na lugha.

Audio Credit:
Assumpta Massoi/Brenda Mbaitsa
Audio Duration:
1'49"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud