Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea Beijing+25 UN-Women yakutanisha vijana Addis Ababa

Kuelekea Beijing+25 UN-Women yakutanisha vijana Addis Ababa

Pakua

Kuelekea miaka 25 tangu kupitishwa kwa mkakati wa Beijing kuhusu masuala ya usawa wa jinsia, shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN-Women limeunda kikosi kazi cha vijana kinachotathmini mkakati huo ili kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa mstari wa mbele kusongesha mkakati huo.

Miongoni mwa vijana hao 30 ni Anika Jane kutoka shirika la kiraia la wanawake vijana katika siasa nchini Kenya ambaye akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amebainisha kile wanachoandaa,

“Tunaangalia serikali zimeanza kuchukua mikakati aina gani kuhakikisha kuwa katika nchi zao wanawake wanaweza kupata faida za usawa wa kijinsia katika sehemu za hospitali, kazi, siasa, na mambo kama hayo. Sasa hivi hatuwezi kuzungumzia kuhusu usawa wa kijinisia bila kuhakikisha kuwa vijana, yaani mwanamke na mwanaume ambaye yuko katika umri wa chini, wanaelewa katika masomo yao kwamba hakuna kitu kama kukaliwa na wanaume. Tunafaa tunachukua vijana, tunawaeleza ya kuwa sasa hivi nafasi zipo sawa kwa kila mtu. Kwa hivyo vijana wanafaa kuwa katika tume yoyote , katika mradi wowote, vijana sio wanufaishwa ambao wanapatiwa mwisho wa mradi ama chochote, lakini ndio wenye kuanzisha mikakati na miradi katika jamii. Vijana ndio wale ambao sasa ndio viongozi si wa kesho tena manake kila siku mnasema kesho , vijana ndio viongozi wa leo na wa sasa.”

Kutoka Tanzania ni Abel Koka wa shirika la kiraia la Restless Development akiwa anahusika na mradi wa Tutimize Ahadi yeye tumemuuliza ushiriki wa vijana mashinani unaweza kuleta mabadiliko gani? Ambapo kijana Koka amesema, “Kwenye jamii zetu vijana wanaunda nguvu kazi kubwa au ni sehemu kubwa ya jamii. Hivyo basi kama vijana watashiriki kwa asilimia 100 kudai usawa wa kijinsia na kudai ukomeshaji wa mimba za utotoni, kudai ukatilii dhidi ya mwanamke, ni dhahiri kwamba tutaweza kufika pale tunapotaka kufika. Kwa mfano, Tanzania sasa hivi rais wetu ameamini sana vijana , vijana wamepewa nafasi kwenye wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa baraza la mawaziri, lakini pia tuna wanawake vijana ambao ni wabunge. Lakini je, ni kazi gani ambayo wanafanya ili kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unafikiwa? Kwa hivyo hiki ni kitu ambacho tunatarajia kupelekwa hizi sauti nyumbani ili kuhakikisha kwamba wao nao wanafanya kazi yao au wanatumia nafasi zao kuhakikisha kwamba yale yote makandokando yote ambayo yanamzuia mwanamke yanamvuta mwanamke na msichana nyuma, yanaondolewa, na wanawake na wasichana, wanapata haki sawa na nafasi sawa kama wanaume na wavulana.”

Kwa upande wake, Doreen Moraa, mwanaharakati kijana kutoka Kenya kuhusu masuala ya Ukimwi, yeye anasema ingawa kuna mafanikio nchini mwake ya vijana barubaru kupata nafasi za uongozi bado kuna pengo la kijinsia akisema, “Bado tuna mapengo ambayo bado hayajapokelewa vizuri. Kwa vile kama wanawake vijana hawajahusishwa sana katika haya mambo ya usawa wa kijinsia na pia sauti zao hazijasikika vile. Katika kazi na vyeo, unapata kwamba wanawake wanaambiwa kwamba labda amehusiana na mwajiri wakw ili apandishwe cheo. Kwa hivyo haifanywi kulingana na ustahili. Kwa hivyo tungependa sana kuishawishi serikali ya Kenya ichague vijana zaidi. Juzi tu tumemwona mwanamke kwenye umri wa miaka 70 akichaguliwa kulisimamia shirika la ajira nchini Kenya. Kama ingekuwa mwanamke barubaru anayeelewa kwamba vijana wana shida ya ukosefu wa ajira, labda mwanamke huyu angeweza kuinua vijana. Kwa hivyo tunafaa kama nchi, kufanya mambo mengi zaidi. Kuna maeneo muhimu ambayo Beijing +25 huwa inaangazia. Na hayo maeneo muhimu, mengi yametajwa mara kwa mara. Lakini, hayajatimizwa sana. Kwa hivyo tunataka tukitoka hapa, haya yatiliwe mkazo yawe halisi ili wakati tunafanya review ya Beijing +25 tuone kwamba wanawake wamepata fursa ya kuenda shule, suala la ukeketaji liishe, na wanawake wengi washirikishwe katika uamuzi kwenye mashirika makuu duniani. Kwa hivyo, tunataka kuona kwamba tukitoka hapa, vile ambavyo wale wanadada walivyoanzisha Beijing +25 ya mwaka 1995, walivyoanza, sisi sasa kama vijana kazi yetu ni kumalizisha hii safari na tuifanye iwe halisi. Yaani ije ikawa hai.”

Maadhimisho hayo ya miaka 25 yatafanyika mwakani.

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Sauti
5'29"
Photo Credit
Warren Bright/UNFPA Tanzania