Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet asema amevunjika moyo na mwelekeo wa haki za binadamu duniani

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet asema amevunjika moyo na mwelekeo wa haki za binadamu duniani

Bachelet akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema ana hofu kubwa ya kwamba dunia hivi sasa imeungana zaidi kuliko wakati wowote ule kiasi kwamba athari za haki za binadamu kwenye eneo moja zinaweza kuwa na madhara makubwa kikanda au kimataifa.

(Sauti ya Michelle Bachelet)

“Tumeshuhudia hili kwa jinsi watu wengi wanakimbia nchi zao kutokana na mizozo, ukosefu wa usalama, ukandamizaji wa kisiasa, majanga ya tabianchi na kushinda kulinda haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.”

Bi. Bachelet pia ametaja kushamiri kwa kauli za chuki, kibaguzi na chuki dhidi ya wageni akisema vinasambaa kwenye kiza cha mitandao ya intaneti na dhahiri kabisa kwenye mitandao ya kijamii.

Amekumbusha kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu ni suala linalopaswa kushughulikiwa na kila mtu kwa kuwa linaathiri kila upande kuanzia amani, usalama, uchumi na hubisha hodi kwenye kila kaya.

Hata hivyo cha kusikitisha amesema mipaka ya nchi inatumika kuzuia ufuatiliaji wa haki za binadamu na hata wao wenyewe ofisi ya haki za binadamu huzuia kufanya hivyo jambo linalomtia hofu.

(Sauti ya Michelle Bachelet)

“Mienendo hii miwili inayoenda pande tofauti inaonekana kutuondoa kwenye suluhu za kimataifa kwenda kwenye matatizo ya kimataifa. Nasihi nchi zishirikiane kutatua masuala ya haki za binadamu kwa njia ya pamoja ya ushirikiano.”

Pakua

Mwaka mmoja baada ya kushika jukumu la ukamishna wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema hakutarajia kuwa itakuwa kazi rahisi, lakini amevunjwa moyo kutokana na mwelekeo wa haki za binadama hivi sasa. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'39"
Photo Credit
UN Photo/Laura Jarriel