Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye manusura 116 wa ajali ya boti waruhusiwa kuteremka kutoka boti ya uokozi huko Sicily.

Hatimaye manusura 116 wa ajali ya boti waruhusiwa kuteremka kutoka boti ya uokozi huko Sicily.

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema manusura 116 wa ajali ya boti ya wiki iliyopita waliokuwa wakishikiliwa hadi leo Jumatano Julai 31 ndani ya boti ya ukozi ya Italia kwenye bandari ya Sicily wameruhusiwa kuteremka kutoka kwenye boti hiyo.

UNHCR inasema manusura hao walioondoka Libya kwa kutumia boti mbili waliokolewa baharini na walinzi wa doria wa Italia Julai 25 na kuhamishiwa katika boti ya walinzi wa pwani ya Bruno Gregoretti.

Awali vyombo vya habari viliripoti ya kwamba Italia imesema boti hiyo isitie nanga kwenye bandari ya Italia hadi pale nchi za EU zitakapokubali kuwachukua abiria wote ndani ya boti hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo  watu  10 waliokuwa wakihitaji matibabu na Watoto 16 waliokuwa wakisafiri peke yao bila wzazi wala walezi wameruhusiwa kutoka nje ya boti hiyo na kupatiwa msaada unaohitajika wakati wengine wakisalia ndani ya boti hiyo hadi pale Mataifa ya EU yatakapokubali kuwachukua.

Msemaji wa UNHCR Charlie Yaxley kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa Twitter amethibitisha tayari kuruhusiwa kwa wahamiaji hao kushuka kutoka boti hiyo ya uokozi  iliyokuwa imetia nanga kwenye eneo la Augusta, mashariki mwa pwani ya Sicily.

Kuanzia Jumatatu wiki hii chama cha msalaba mwekundu nchini Italia kimekuwa kikiwapa manusura hao vifaa vya kujisafi, nguo na viatu.

Shirika la UNHCR limekuwa likitoa wito wa ushirikiano mara kadhaa miongoni mwa nchi za EU ili kuhakikisha manusura hao waliokolewa baharini wanatolewa kwa usalama ndani ya boti na kusaidiwa kwa misingi ya sheria za kimataifa za wakimbizi na wahamiaji.

Audio Credit
Grace Kaneiya/ Assumpta Massoi
Audio Duration
1'45"
Photo Credit
UNHCR/L.Boldrini