Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto ya kupambana na Ebola DRC ni fedha:UNICEF

Changamoto ya kupambana na Ebola DRC ni fedha:UNICEF

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema litahitaji kuongeza mara tatu bajeti yake ili kufanikisha operesheni zake kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ambayo yanakabiliwa na mlipuko wa Ebola sambamba na surua.  Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

Kauli hiyo ya UNICEF imetolewa hii leo na mtaalamu wake wa afya Jerome Pfaffman baada ya ziara yake ya tatu nchini DRC ambako ameshuhudia jinsi ambavyo maeneo hayo yanakabiliwa na dharura ya afya ya umma kutokana na magonjwa hayo sambamba na ukosefu wa usalama unaokwamisha operesheni dhidi ya magonjwa hayo.

Bwana Pfaffman amesema takribani nusu ya vituo vya afya vimesambaratishwa kutokana na mapigano  yaliyodumu kwa miaka miwili sasa, idadi kubwa ya watu wamekimbia makazi yao.

Hata hivyo amesema “tumefanikisha awamu ya kwanza ya kampeni ya chanjo dhidi ya surua huko Bunia lakini tunahitaji kupatia chanjo watoto wengine 40,000 dhidi ya magonjwa hatari.”

Amesema ni kwa mantiki hiyo mpango mkakati wao mpya unajumuisha kuimarisha hatua za kiafya na kukidhi mahitaij ya kibinadamu na kijamii na ndio msingi wa ombi lao la jumla ya dola milioni 170.

“Dola milioni 70 ni kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya milipuko, dola milioni 30 kujenga uwezo wa jamii kwenye maeneo yenye hatari na dola milioni 70 kwa ajili ya kusambaza huduma muhimu,” amefafanua mtaalamu huyo wa afya wa UNICEF.

Tangu kulipuka kwa Ebola mwaka jana hadi tarehe 28 mwezi huu wa Julai, wagonjwa 2,671 wamethibitishwa kuugua Ebola miongoni mwao 700 ni watoto ambao zaidi ya nusu wan aumri wa chini ya miaka mitano.

“Zimesalia siku mbili kabla ya kutimiza mwaka mmoja tangu mlipuko wa Ebola DRC, kwa hivyo lazima tuchukue hatua mlipuko huuusitimize miaka miwili,” ametamatisha Bwana Pfaffman.

Audio Credit
UN News/ Assumpta Massoi
Audio Duration
1'46"
Photo Credit
Finnish Red Cross/Maria Santto