Bado makundi muhimu hayapati huduma za kujikinga na VVU na Ukimwi- Ripoti

16 Julai 2019

Kasi ya maendeleo ya kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi, VVU, kasi ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa dawa na kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi inapungua, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ukimwi, UNAIDS.  Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Nchini Afrika Kusini katika kitongoji cha Tembisa kilichopo mji mkuu wa kibiashara, Johannesburg, harakati zikiendelea za maisha wakati huu ambapo UNAIDS imetoa ripoti yake ikitaja kuwa taifa hili limesonga mbele kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 40.

Afrika Kusini ikifanikiwa, mataifa mengine yamekumbwa na mkwamo katika kutokomeza Ukimwi.

Ripoti inaonesha kuwa watu wanaojidunga madawa, mashoga, waliobadili jinsia, makahaba na wafungwa ni asilimia 95 ya maambukizi mapya ya VVU huko Ulaya Mashariki, Asia ya Kati, Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Ingawa hivyo ni chini ya asilimia 50 tu ya watu hao ndio wanapata dawa ikimaanisha kuwa bado wananyanyapaliwa katika huduma dhidi ya VVU.

Nchini Burkina Faso nako wamebaini kundi lililosahauliwa ni vijana kama asemavyo Christine Kafando, muasisi wa shirika la kiraia linalokabiliana na Ukimwi, AED ambaye anasema kwamba, “tulibaini kuwa idadi kubwa ya waathirika wa VVU hii leo ni vijana wenye umri kati ya miaka 14 na 24 na haikubaliki kuwa baada ya uhamasishaji wa miaka kadhaa na usaidizi! Tunawezaje kusahau kizazi hiki?”

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo huko Eshowe nchini Afrika Kusini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Gunilla Carlsson amesema kuwa kinachohitajika hivi sasa ni kuchagiza uongozi wa kisiasa katika kutokomeza Ukimwi kwa kuwekeza vya kutosha na kwa uhakika, na kwa kuangalia kile kinachofanya baadhi ya nchi kufanikiwa kwenye vita hiyo.

Mwaka 2018 pekee, kulikuwepo na watu wapya milioni 1.7 walioambukizwa VVU, ikiwa imepungua kwa asilimia 16 tangu mwaka 2010.

Audio Credit:
Assumpta Massoi/Jason Nyakundi
Audio Duration:
2'14"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud