Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchungaji aliyebainika kuwa na Ebola DRC sasa anapatiwa matibabu- WHO

Mchungaji aliyebainika kuwa na Ebola DRC sasa anapatiwa matibabu- WHO

Pakua

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limechukua hatua kufuatia kubainika kwa mgonjwa wa Ebola kwenye mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Flora Nducha na taarifa zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha kujadili mlipuko wa Ebola unaoendelea huko DRC ambao tangu mwezi Agosti mwaka jana umekumba wagonjwa 2500 na 1665 kati yao wakifariki dunia.

Akizungumzia kisa hicho kipya cha ebola huko Goma, Dkt. Tedros amesema ni mchungaji aliyesafiri kutoka Butembo na kwamba,

“Ingawa kisa hiki kinatia hofu, ni jambo ambalo sisi na serikali tulitarajia na tulishajiandaa. Takribani watu 3000 wamepatiwa chanjo, na mchungaji anapatiwa tiba kwenye kituo kinachoendeshwa na Wizara ya Afya na MSF.”

Hata hivyo Dkt. Tedros amesema,

"Kubainika kwa kisa cha Ebola mjini Goma, kunaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye mlipuko huu. Goma ni mji wa watgu milioni 2 karibu na mpaka na Rwanda na ni lango la ukanda na dunia. Tunaamini mikakati tuliyoweka kudhibiti mlipuko, lakini hatuwezi kuwa makini sana. Kwa mantiki hiyo basi nimeamua kuitisha tena haraka iwezekanavyo kikao cha kamati ya dharura kuhusu afya  ili itathmiini maendeleo ya mlipuko huu na inishauri kadri iwezekanavyo.”

Wakati wa kikao hicho, Waziri wa Afya wa DRC, Dokta Oly Ilunga ametaja mambo muhimu matano ambayo serikali na wadau wake yakiwemo  mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo wanazingatia kudhibiti mlipuko kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuna rasilimali fecha na watu za kutosha ili kuepusha kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo.

Naye Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa masuala ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock amekumbushia umuhimu wa usalama kwenye maeneo ya mlipuko ambako vikundi kadhaa vilivyojihami vimeshamiri na siyo tu kutishia hata kuua watoa huduma, akigusia watendaji wawili ambao waliuawa hivi karibuni huko Butembo.

Kwa mantiki hiyo Bwana Lowcock amekumbusha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa juu ya  umuhimu wa ujumbe wa umoja huo nchini DRC, MONUSCO akisema kuwa wakati mustakabali wa MONUSCO unajadiliwa, ni lazima nchi hizo zizingatie athari za kupunguzwa kwa ukubwa wa ujumbe wa MONUSCO katika harakati za kudhibiti Ebola.”

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
Finnish Red Cross/Maria Santto