Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Nigeria waitikia wito wa UNHCR wa kupokea wakimbizi

Wananchi wa Nigeria waitikia wito wa UNHCR wa kupokea wakimbizi

Pakua

Nchini Nigeria, wakimbizi kutoka Cameroon ambao wanazidi kumiminika nchini humo kutokana na ghasia nchini mwao wanaendelea kupata faraja kutokana na mshikamano kutoka kwa wenyeji wao ambao wameitikia wito wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR wa kuwasihi wafungulie milango wakimbizi. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Sifahamu ningalikuwa wapi! Ni Susan Agbo mkimbizi huyu kutoka Cameroon akiwa kwenye makazi ya mwenyeji wake nchini Nigeria.

Susan anaonekana akibeba benchi la kukalia, kijasho chembamba kikimtoka huku wajukuu zake wakimwangalia.

“Nilipokuja Nigeria, niliishi na wawtu. Baada ya wiki mbili nilihamia kwingine, huko niliishi mwezi mmoja. Nilihamia upande mwingine ambako niliishi mwezi mmoja au wiki mbili kabla ya kuja hapa.”

Ghasia kaskazini-magharibi na kusini-magharibi mwa Cameroon zimesababisha wakimbizi wa ndani 437,000, huku wengine zaidi ya 36,000 wakielekea nchi jirani hususan Nigeria ambako baadhi yao kama Susan wamepata mwenyeji Lucia Ikuru, ambaye ni mjane. 

Wakiwa wanafanya kwa pamoja kazi za nyumbani, Lucia ambaye amemhifadhi Susan na wajukuu zake kwa zaidi ya mwaka sasa na anasema..

“Chochote kidogo nipatacho nampatia. Iwapo mwanamke  huyu ataenda kuishi mahali na jambo lolote baya limfike, sitafurahi. Sasa ni na furaha yuko nami hapa.”

Ambao wamekosa wenyeji, wanaishi kwenye kambi ambapo Josiah Flomo, mkuu UNHCR ofisi ya Ogoja anasema,  “UNHCR imewapatia msaada wakimbizi kwenye makazi na wale ambao wanaishi na wenyeji.”

Audio Credit
Arnold Kayanda/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'49"
Photo Credit
UN News/Daniel Dickinson