Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za ukatili wa kingono hudumu vizazi na vizazi- UN

Athari za ukatili wa kingono hudumu vizazi na vizazi- UN

Pakua

Ukatili wa kingono katika mizozo ni tishio kwa usalama wetu sote na ni doa katika utu wetu amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Arnold Kayanda na taarifa kamili

Kupitia ujumbe wake maalumu wa siku ya kimataifa kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kingono katika mizozo Guterres amesema ukatili huo unatumika kama mbinu ya vita kutisha watu na kusambaratisha jamii na kwamba “athari zake zinaweza kwenda vizazi na vizazi kupitia madhila, unyanyapaa, umasikini, athari za kiafya za muda mrefu na mimba zisizotakikana. Katika siku ya kimataifa kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kingono katika mizozo tunapaswa tuwasikilize waathirika na kutambua mahitaji na matakwa yao.”

Ameongeza kuwa wengi wa waathirika hao ni wanawake na wasichana lakini pia wanaume na wavulana, ambao wanahitaji msaada ili kupata huduma za afya za kuokoa maisha yao, kujikimu kimaisha, haki na fidia.

Na kwa mantiki hiyo Umohja wa Mataifa katika operesheni zake mbalimbali umeanzisha mafunzo maalum kwa ajili ya waathirika hao matahalani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, kupitia mpango wake nchini MONUSCO. Mafunzo hayo ni ya ujasiriamali wa aina mbalimbali kuanzia ufugaji, upishi, kuoka mikate, na hata ushonaji. Miongoni mwa waliofaidika na miradi hiyo ni kina mama hawa muoka mikate na fundi cherahani.

Umoja wa Mataifa unasema katika kuadhimisha siku hii pia tunawaenzi ambao wanafanyakazi mstari wa mbele, wakiwasaidia moja kwa moja waathiri ili kujenga upya maisha yao.

Katibu Mkuu ametoa wito kwamba hatua za pamoja lazima zijumuishe maamuzi ya pamoja ili kuhakikisha uwajibikaji kwa waliotekeleza ukatili huo na kushughulikia kutokuwepo usawa wa kijinsia ambao unachochea maovu haya kwani kwa pamoja dunia inaweza na inapaswa kubadili ukwepaji sheria kwa kuweka haki, na kutofautiana kwa kuchua hatua.

Audio Credit
Flora Nducha/Arnold Kayanda
Audio Duration
2'25"
Photo Credit
MONUSCO