Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi Uganda wazungumzia harakati dhidi ya Ebola

Wananchi Uganda wazungumzia harakati dhidi ya Ebola

Pakua

Mamlaka za wilaya mbalimbali za mpakani kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zimeimarisha juhudi za uhamasishaji wa jamii kuhusu tishio kufuatia mlipuko wa Ebola na njia za kinga baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine 10 waliokutana na marehemu hao wakiendelea kufanyiwa uchunguzi katika wilaya ya Kasese. 

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini Uganda, John Kibego alitembelea maeneo ya wilaya za Pakwach na Buliisa ilikuona hali halisi na kuzungumza na wakazi miongoni mwao ni William Rwenjema, mkazi wa eneo lililo umbali wa kilometa 2 kuingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Bwana Rwenjema anasema kuwa, "anaona kuna mashine zimewekwa za kupima na kwingine hajaona na hivyo anaingia na hofu." Mkazi mwingine ambaye hakujitambulisha amesema kuwa miongoni mwa mambo wanafundishwa ni kusalimiana" hupaswi kusalimia mwenzako mkononi, nyanyua tu mkono kutoka mbali." 

Kwa upande wake serikali ya Uganda na wadau wake imesema kuwa, "tumeweka maeneo manne mpakani ya uchunguzi ambako kuna madaktari wanaofanya kazi mchana na usiku," amesema Hunnington Tibaijuka, afisa anayehusika na uelimishaji jamii kuhusu masuala ya afya na pia afisa wa mawasiliano wilayani Buliisa. 

Amesema wameshafundisha watu 1,600 ambao wanapita nyumba kwa nyumba na shule kuelimisha watu kuhusu jinsi ya kujikinga dhidi ya Ebola. 

Viongozi wa dini nao hawakuachwa nyuma wakisema kuwa nao pamoja na kusongesha neno la Mungu, wanaelimisha waumini wao kuchunga afya zao wakiwaambia kuwa  Ebola ipo karibu na hivyo ianweza kuingia kwao.

Hata hivyo Bwana Tibaijuka anasema kuna changamoto, ikiwemo mmiminiko wa wakimbizi na mipaka isiyo rasmi akisema kuwa. "watu wengine wanaingia kupitia upande mwingine bila wao kufahamu na hata kumpima."

Naye Janet Oduokachen, mchuuzi wa samaki kutoka Panyimol, soko kubwa zaidi la samaki magharibi na kaskazini mwa nchi, ambalo huvutia wanunuzi kutoka Jamhuri ya Afrika  ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Sudan Kusini anasema kuwa, "biashara mimi  nafanya hapa na pia nafanya DRC.  Maeneo ya Bunia kama kilometa 200. Wengine wanatoka kule kwenye Ebola na hata hapa Panyimol wanaingia."

 

Audio Credit
Flora nducha/John Kibego
Audio Duration
2'48"
Photo Credit
World Bank/Vincent Tremeau