Wilaya za Kisarawe na Kibaha nchini Tanzania ni mfano dhahiri wa ujumuishi wa watoto wenye ulemavu- ADD International

Wilaya za Kisarawe na Kibaha nchini Tanzania ni mfano dhahiri wa ujumuishi wa watoto wenye ulemavu- ADD International

Pakua

Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa watu wenye ulemavu, CRPD ukiingia siku ya pili kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, wilaya za Kisarawe na Kibaha mkoani Pwani nchini Tanzania zimetajwa kuwa mfano wa mafanikio ya sera za ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika nyanja ya elimu. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Jimmy Innes, Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la kiraia, ADD linalosaidia kujenga uwezo wa mashirika ya watu wenye ulemavu, ametaja mafanikio hayo akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa mkutano huo.

Bwana Innes amesema katika wilaya hizo za Kibaha na Kisarawe…

« Tumefanya kazi kwa zaidi ya miaka mitatu, na taratibu tunapiga hatua ndogo ndogo moja kwa moja mpaka tumefika hatua ambapo viongozi wa halmashauri wameelewa wa hiki tunaita elimu jumuishi. Na sasa imefika wakati viongozi wa halmashauri wenyewe wanaanza kuahidi na kutekeleza bajeti ya elimu jumuishi inaongezeka kutoka mfuko wa halmashauri. Kwa hii mimi naona ni hatua kubwa sana.»

Na ujumbe wa ADD kwa mkutano huo wa wiki mbili ni nini?

“Tunasema kwamba haki za watu wenye  ulemavu, ni lazima tujenge uwezo wa watu wenye ulemavu kudai haki zao wenyewe. Si kwamba haki ni kitu cha kupewa, hapana! Haki ni kitu cha kudai wewe mwenyewe upate haki yao. Kwa hiyo hiyo ujumbe wetu kwa mkutano huu na mapambano ya haki kwa jumla ni lazima tuwape watu nafasi waweze kudai haki zao wenyewe.”

Alipoulizwa amepokea vipi hatua ya Umoja wa Mataifa kutangaza mkakati wake wa ujumuishaji watu wenye ulemavu kuanzia kwenye ofisi zake za makao makuu hadi mashinani, Bwana Innes amesema “kwa upande mmoja najisikia vizuri kuwa Umoja wa Mataifa umechukua hatua hiyo, lakini tunajiuliza mwaka huu wa 2019 mpaka leo ndio umezindua mkakati huo? Si kwamba umechelewa lakini tunatakiwa kufanyia kazi kwa dhati.”

Audio Credit
Arnold Kayanda/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'57"
Photo Credit
© UNICEF/Pirozzi