Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Benki ya Dunia kusaidia Dar es salaam kukabiliana na mafuriko

Mradi wa Benki ya Dunia kusaidia Dar es salaam kukabiliana na mafuriko

Pakua

Kufuatia mafuriko ya mara kwa mara kwenye jiji la Dar es salaam nchini Tanzania, Benki ya Dunia imedhamini mradi wa kuwezesha wataalamu kutumia mbinu za kisayansi za kuchambua udongo ili kukabiliana na mafuriko. Taarifa zaidi na Amina Hassan. 

Nchini Tanzania katika jiji la Dar es salaam, mmomonyoko wa udongo ni moja ya visababishi vikubwa vya mafuriko ambayo yamekuwa si tu chanzo cha vifo bali pia huharibu miundombinu.

Mradi wa Benki ya Dunia kwa ajili ya miji yenye mnepo unatumia zana na ujuzi wa ndani ya nchi kuchambua na kuunda ramani ya udongo ambayo itatoa taarifa za hatua za kuchukua kupambana na mafuriko na pia kwa ajili ya mipango miji ya jiji la Dar es salaam.

Mussa Natty, Mkurugenzi wa zamani wa Manispaa ambaye pia ni mtaalamu wa miji anasema, “Kuna takataka nyingi zinazokuja na mmonyoko, hiyo ndiyo sababu tuna mafuriko kwa sababu sasa maji hayatiririki katika kiwango cha kawaida kuelekea baharini. Watu maskini wanaoishi katika bonde la msimbazi ndio walio hatarini zaidi. »

Ufanisi wa ufuatiliaji mafuriko na upimaji vinahitaji data sahihi za udongo ambapo jiji la Dar es salaam linatumia wanasayansi watanzania kuuchambua udongo.

Wataalamu ni 16 katika maeneo 643 ya kimkakati na tayari kilomita za mraba 2752 zimewekwa katika ramani.  Sia Salonga, ni mtaalamu mchambuzi wa udongo na ramani. “Ninajivunia sana sana kuwa mmoja wa washiriki. Tunatumia ramani kufika katika eneo na baada ya kufika huko tunaanza kuchimba eneo na baadaye tunajaza taarifa katika kifaa cha kutunzia data yaani.”

Naye Felister Tobias anaeleza zaidi kazi inavyofanyika akisema kuwa “Baada ya kukausha udongo, tunaupima kisha tunauchekecha, baada ya kuuchekecha tunapima uzito wa udongo kisha tunauweka katika ODK.”

Watafiti wamerekodi zaidi ya aina 600 tofauti za udongo na ramani kamili ya udongo ya jiji sasa inaeleza  hatua za kuchukua kudhibiti mafuriko na pia mipango bora ya miji.

Sia Salonga anasema hii itawasaidia kufahamu kuwa mathalani eneo fulani ni rahisi kumomonyoka. Mussa Natty anahitimisha, “Taarifa tunazozipata kutoka kwenye udongo, zitatusaidia kufahamu umbo la mto, jambo muhimu sana kwetu katika kulishughulikia eneo na pia kwa ajili mipango ya matumizi ya ardhi katika siku zijazo.”

Audio Credit
Arnold Kayanda/ Amina Hassan
Audio Duration
2'11"
Photo Credit
Benki ya Dunia/Screenshot