Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano kati ya polisi wa taifa na UNPOL unasaidia ulinzi wa raia DRC

Ushirikiano kati ya polisi wa taifa na UNPOL unasaidia ulinzi wa raia DRC

Leo ni siku ya walinda amani duniani ambapo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, polisi wa Umoja wa Mataifa UNPOL wanashirikiana na polisi nchini humo, PNC katika kuhakikisha ulinzi wa raia. 

Nchini DRC kuna polisi 2,000 kutoka nchi mbalimbali ambao wanaunga mkono shughuli za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wakifanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuhakikisha ulinzi wa raia hii ikiwa ndio wajibu mkuu wa polisi wa Umoja wa Mataifa kama anavyosema kamishna wa polisi, MONUSCO, Jenerali Awale Abdounasir.

(Sauti ya Awale)

“Askari polisi wa MONUSCO tumeweka mikakati kuhusu mbinu za kutekeleza ulinzi wa amani. Tumebuni mbinu za kukabiliana na ukosefu wa usalama mashinani na hili linatuwezesha kufanya kazi kwa karibu na vikosi vya polisi la taifa. Tumefanya kazi kwa pamoja kupunguza ukosefu wa usalama katika baadhi ya miji mashariki mwa nchi, ambako kwa pamoja tumeanzisha mpango uliopewa jina SOLI ambao ulibuniwa na kutekelezwa na umepata mafanikio tangu mwaka 2018.”

 Miji ambayo imepata faida na mkakati wa SOLI ni Oicha, Beni, Goma, Bunia, Uvira, Kalemie na Bukavu. 

Mpango wa SOLI unatoa taarifa kwa wenyeji kuelewa kuhusu usalama wao na hutoa namba ambayo wanaweza kupiga iwapo kuna hofu ya usalama. 

Kwa mantiki hiyo UNPOL na PNC wameweka ofisi katika maeneo mbalimbali kote nchini DRC kwa lengo hilo moja la ulinzi wa raia. Jenerali Placide Nyembo Ngalusha ni kamishna wa polisi wa serikali ya DRC jimboni Kivu Kasakzini.

(Sauti ya Nyembo)

“Nadhani kufikia sasa, ushirikiano umekuwa na matokeo chanya kwa sababu katika ushirikiano huo kikosi cha taifa cha polisi kimekuwa ni mnufaika mkubwa. Kuhusu doria za pamoja na MONUSCO mjini Goma na  kwingineko, tunafanya kazi kwa pamoja kufanikisha SOLI katika kitengo cha kuratibu opereshen na katika kutoa mafunzo, na tunanufaika na  UNPOL kutokana na ushirikiano na mafunzo kwetu.”

Pakua

Leo ni siku ya walinda amani duniani ambapo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, polisi wa Umoja wa Mataifa UNPOL wanashirikiana na polisi nchini humo, PNC katika kuhakikisha ulinzi wa raia. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'1"
Photo Credit
UNMISS