Heko MINUSCA kwa ujenzi wa madaraja sasa tunalala majumbani- Wananchi CAR

28 Mei 2019

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, madaraja yaliyojengwa kwa ufadhili wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSCA, yamesaidia kuimarisha doria zinazofanywa na walinda amani wakiwemo wale wanaotoka Tanzania na hivyo kuimarisha usalama na kurejesha matumaini kwa wakazi wa maeneo ya Gamboula na Noufou. John Kibego na ripoti kamili.

Katika barabara ya kutoka mji wa Gamboula ulioko jimbo la Mambéré-Kadéï nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ikiwa ni ya kuelekea mji wa Noufou, walinda amani kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSCA wakivuka daraja huku wakazi wa eneo hilo wakitazama doria hii.

Doria hizi ni muhimu kwa kuzingatia kuwa wakazi wa eneo hili wameshuhudia mashambulio kutoka kikundi kilichojihami cha Siriri ambacho kimetia moto nyumba za wanakijiji.

Meja Christophe Buchue, wa kikosi cha Tanzania MINUSCA anasema tangu wahamishie doria zao kutoka Gamboula hadi Bila Poli, hali ya usalama ni tulivu lakini haitabiriki na ukosefu wa madaraja thabiti umekuwa ukisababisha barabara hiyo isipitike.

Hata hivyo amesema, "eneo hili lina misitu minene kuanzia Gamboula hadi Bila Poko, na madaraja mengi yamejengwa kwa mbao. Hata hivyo sasa tunatumia vifaa thabiti vya ujenzi, kwa hiyo tunahitaji madaraja yaliyojengwa kwa saruji ili tuweze kufanya doria zetu kwa urahisi zaidi kutoka Gamboula hadi Bila Poko na kutoka Bila Poko hadi Noufou".

Hata mamlaka za mji wa Gamboula zimetambua umuhimu wa madaraja hayo katika kuimarisha  usalama na doria huku Samuel Sambo ambaye ni mkulima, naye akifunguka akisema,"kabla ya ujenzi wa hili daraja, hatukuweza kabisa kulala kwenye nyumba zetu. Lakini MINUSCA wamejenga hili daraja na sasa tuna faraja zaidi. Tunalala na tuna chakula.”

Audio Credit:
Flora Nducha/John Kibego
Audio Duration:
1'52"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud