Tuwekeze zaidi kwenye ulinzi wa amani ili kuokoa raia na walinda amani wetu- Guterres

Tuwekeze zaidi kwenye ulinzi wa amani ili kuokoa raia na walinda amani wetu- Guterres

Pakua

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kumefanyika maadhimisho ya siku ya walinda amani duniani ikienda sambamba na utoaji wa nishani kwa walinda amani waliopoteza maisha wakihudumu kwenye sehemu ya mizozo. Amina Hassan na maelezo zaidi.

Tukio  hilo limeongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambapo kwanza ameweka shada la maua kukumbuka walinda amani wote waliopoteza maisha tangu kuanza kwa ulinzi wa amani wa umoja huo mwaka 1948.

Kisha akakabidhi medali ya ujasiri wa kipekee ya Kapteni Mbaye Diagne kwa  familia ya mlinda amani kutoka Malawi, Chancy Chitete of Malawi ambaye aliuawa wakati wa operesheni dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces, ADF huko Kivu Kaskazini ambapo alimuokoa askari kutoka Tanzania.

Akimzungumzia Chitete, Katibu Mkuu amesema kwamba,

“Tunatoa heshima zetu kwa Chancy CHITETE, mlinda amani raia wa Malawi ambaye wakati akihudumu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC alifariki dunia wakati akijaribu kuokoa maisha ya mlinda amani mwenzake.”

Hivyo amesema kwamba,

"Ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni uwekezaji muhimu katika amani na usalama duniani. Hata hivyo unahitaji ahadi thabiti ya kimataifa. Na ndio maana tumezindua Hatua kwa Ajili ya Ulinzi wa Amani, mpango ambao unalenga kufanya ujumbe wa ulinzi wa amani kuwa thabiti, salama na uendane na mazingira ya siku zijazo”.

Luteni Daudi Makamba, kamanda wa kikosi cha sita cha vikosi maalum ni miongoni mwa waliokuwepo wakati wa shambulio hilo la tarehe 14 mwezi Novemba akiwa kiongozi wa kikosi maalum ambapo amesema kilichotokea..

(Sauti ya Luteni Daudi Makamba)

“Kweli tulipofika maeneo ya Kididiwe tulikutana na adui tuliweza kumpiga na kumnyong’onyesha kabisa. Katika mapigano hayo makali nilipoteza askari wangu mmoja, na mwingine alipigwa risasi ya mguu na mimi mwenyewe nilipigwa risasi ya bega.”

Na je kwa tukio hilo amejifunza nini?

(Sauti ya Luteni Daudi Makamba)

 “Nimejifunza katika uwanja wa medani, nidhamu, ushirikiano na umoja ni kitu cha muhimu sana.”

Utoaji wa tuzo hiyo ya Mbaye Diagne umeenda sambamba na utunuku wa medali ya Dag Hammarskjöld kwa wanajeshi, polisi na watendaji wa kiraia waliopoteza maisha wakati wa ulinzi wa amani mwaka 2018 hadi mwezi Machi mwaka huu wa 2019. Miongoni mwao ni 5 kutoka Tanzania waliouawa wakati wakihudumu Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Audio Credit
Grace Kaneiya/Amina Hassan
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
UN/Eskinder Debebe