Dkt Agnes Kijazi: Hali ya hewa haina mipaka, ni muhimu nchi zote tushirikiane.

Dkt Agnes Kijazi: Hali ya hewa haina mipaka, ni muhimu nchi zote tushirikiane.

Mkutano wa sayansi, teknolojia na ubunifu unakunja jamvi hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo wabunifu wa sayansi na wabobevu wa teknolojia wamejadiliana kwa siku mbili.  Miongoni mwao ni Dkt Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania ambaye ni mmoja wa wajumbe 10 wa jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa la kutoa ushauri kuhusu jinsi sayansi na teknolojia inavyoweza kutumika kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Katika mahojiano na Idhaa hii ya Umoja wa Mataifa ametueleza kuwa nchi zinakubaliana kushirikiana kwa kuwa uharibifu katika nchi moja, kunaweza kusababisha mabadiliko ya tabia nchi katika nchi nyingine.

Dkt Kijazi anaanza kwa kueleza kile kinachoendelea katika chumba cha mikutano, “mkutano wa mwaka huu ni mkutano muhimu kwani tunakuwa na wabunifu ambao wamebuni vitu mbalimbali vinavyosaidia kwenye maendeleo endelevu, SDGs lakini pia tunakuwa na watu ambao wanakuwa wamebobea katika sayansi.” 

Dkt Kijazi ambaye pia katika mkutano huu ni mwenyekiti mwenza anaeleza namna ambavyo nchi yake ya Tanzania imejipanga, “ Tanzania tumejipanga vizuri tunayo tume ya sayansi na teknolojia Tanzania COSTECH. Kwa hivyo wanasayansi wengi ambao wako nchini kupitia COSTECH wanapata nafasi ya kufanya utafiti  na kuweza kutoa matokeo ya utafiti wao kupitia COSTECH. Lakini Tanzania ni wajumbe wa shirika la kimataifa linaloangazia masuala ya mabadiliko ya tabianchi lililo chini ya Umoja wa Mataifa.”

Mtaalamu huyo aliyebobea katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa, anasema hivi sasa mataifa yote yanahamasisha ushirikiano ili kutafuta suluhu ya pamoja, “hali ya hewa haina mipaka, kwa hiyo jambo linguine linalotokea duniani katika sehemu nyingine linaweza likaathiri nchi yetu. Na ndilo hilo linalotokea. Kwa hiyo mambo ya ushirikiano katika masuala haya ya mabadiliko ya tabia nchi ni ya muhimu sana. Na ndiyo maana mkutano kama huu wa Umoja wa Mataifa, nchi zinakaa zote kwa pamoja ili kuangalia sasa tufanye nini ili kuhakikisha kwamba tunaweza kupunguza athari ambazo zinatokea. Na zile nchi ambazo zinapata athari kubwa zaidi lakini unakuta kwamba wao hawazalishi zaidi hata gesi ukaa katika nchi yao, tufanye nini ili tuweze kuwasaidia, ndiyo mambo hasa yanayojadiliwa katika mikutano mbalimbali ya Umoja wa Mataifa.”

Pakua

Mkutano wa sayansi, teknolojia na ubunifu unakunja jamvi hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo wabunifu wa sayansi na wabobevu wa teknolojia wamejadiliana kwa siku mbili.  Miongoni mwao ni Dkt Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania ambaye ni mmoja wa wajumbe 10 wa jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa la kutoa ushauri kuhusu jinsi sayansi na teknolojia inavyoweza kutumika kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Katika mahojiano na Idhaa hii ya Umoja wa Mataifa ametueleza kuwa nchi zinakubaliana kushirikiana kwa kuwa uharibifu katika nchi moja, kunaweza kusababisha mabadiliko ya tabia nchi katika nchi nyingine.

Audio Credit
Arnold Kayanda
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
WFP/Photolibrary