Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa inaweza kusaidia kutegua kitendawili cha zahma ya wakimbizi.

Sanaa inaweza kusaidia kutegua kitendawili cha zahma ya wakimbizi.

Sanaa inaweza kuwa moja ya nyezo ya kutanabaisha madhila yanayowakumba wakimbizi duniani, na ndio maana shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema maonyesho mapya ya sanaa ya mwaka huu Venice Biennale yalilenga kuliweka suala la wakimbizi katikati ya mjadala wa endapo sanaa ijaribu kubadili mtazamo wa jamii kuhusu wakimbizi. 

Katika mji wa Venice nchini Italia mji ambao ni mashuhuri kwa maonyeshi ya kazi za sanaa, zaidi ya watu 100 wamekusanyika kwenye ufunguzi wa maonyesho ya Rothko kwenye ufukwe wa Lampedusa.

Sanaa zinazoonyeshwa ni kazi za watu maarufu kimataifa kama vile Ai Weiwei na Richard Moss lakini pia wasanii chipukizi ambao ni wakimbizi kutoka Syria, Iran, Iraq, Corte D’voire na Somalia.

Maonyesho haya yamefanikishwa na UNHCR, na Carlotta Sami ni msemaji wa shirika hilo kwa Ulaya Kusini anasema, hii ni njia ya kuonyesha utu wa binadamu ambao wamelazimika kufungasha virago na kuhama makwao na pia ni njia ya kujenga daraja miongoni mwa dunia, hasa ulimwengu wa sanaa ambao unapenya kila kona ya jamii duniani na kuongeza kuwa hii

(SAUTI YA CARLOTTA SAMI- GRACE)

“Ni fursa ya kutafakari kuhusu ubinadamu, hali ya ubinadamu katika hali zote zinazotafsiriwa na bila shaka uhamiaji unachukuliwa kuwa moja ya mada kuu inayoghubika ubinadamu wetu siku hizo”

Kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ya Binnale “Na uishi katika nyakati za kuvutia” ikilenga kuchagiza masuala ya kijamii mojawapo likiwa ni jinsi Ulaya inavyokabiliana na mgogoro wa wakimbizi.

Na miongoni mwa wakimbizi ambao kazi zao za sanaa zinaonyeshwa wamelizungumzia suala la ukimbizi na uhamiaji katika njia mbalimbali, Majid Aid kutoka Iran hivi sasa anaishi Uingereza ameonyesha video ya vikaragosi vya familia ikipitia safari ya machungu nchi kavu na baharini. Mohammed Keita aliyekimbia Corte D’voire ameonyesha picha alizopiga mitaani kwenye maskani yake mapya nchini Italia. Na kwa Rasha Deep msanii kutoka Syria ambaye sasa ni mkazi wa Ujerumani nyumbani atokako ndiko alikokumulika

(SAUTI YA RASHA DEEP- AMINA )

“Vita ndio tatizo langu kubwa na ndio ujumbe wangu mkubwa, sio wakimbizi, sababu ya vita ndio maana kuna wakimbizi, kama hakuna vita hakuna wakimbizi, na sihitaji kukimbia nchi yangu, kwa nini?

Rothko Lampedusa ni maonyesho pekee yaliyojikita na suala la wakimbizi, lakini sio maonyesho pekee yanayoshughulikia suala la wakimbizi. Katika aeneo la Arsenale kunakofanyika maonyesho makubwa ya mji huo boti iliyozama Mediterranea Aprili mwaka 2015 na kukatili maisha ya wakimbizi na wahamiaji takriban 800 imewekwa kwenye maonyesho.

Pakua

Sanaa inaweza kuwa moja ya nyezo ya kutanabaisha madhila yanayowakumba wakimbizi duniani, na ndio maana shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema maonesho mapya ya sanaa ya mwaka huu Venice Biennale yalilenga kuliweka suala la wakimbizi katikati ya mjadala wa endapo sanaa ijaribu kubadili mtazamo wa jamii kuhusu wakimbizi. 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
UN News Kiswahili/ Grece Kaneiya