Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha mapokezi cha UNHCR mjini Maicao Colombia, mkombozi kwa maelfu ya wavenezuela.

Kituo cha mapokezi cha UNHCR mjini Maicao Colombia, mkombozi kwa maelfu ya wavenezuela.

Pakua

Kituo cha mapokezi kilichofunguliwa mwezi uliopita na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, mjini Maicao nchini Colombia, kimekuwa mkombozi kwa maelfu ya wakimbizi kutoka Venezuela wanaokimbia hali ngumu nchini mwao. 

Mji wa Maicao ukiwa na takribani wakazi 100, 000, hivi sasa unawahifadhi wakimbizi na wahamiaji wapatao 30,000. Miongoni mwao ni Darlys na watoto wake wawili.

Katika tathimini iliyofanywa na UNHCR mwezi Februari, ilionesha kuwa nusu ya wavenezuela 3,500 waliohojiwa walikuwa wanaishi mitaani au katika makazi yasiyo rasmi ndani nay a mji na katika maeneo jirani.

Maelfu ya familia kutoka Venezuela ambao wanafika Maicao wanafika wakiwa nauhaba wa mahitaji ya kuweza kuishi, na wakati mwingine wanafika wakiwa hawana chochote.

Darlys anasema mara ya kwanza aliingia Colombia akiwa peke yake lakini hali ya afya ya mwanae wa kiume anayeugua figo ilizidi kuwa mbaya.

(Sauti ya Darlys)

“Niliamua kuwaleta watoto wangu kwasababu, mtoto wangu wa kiume alikuwa anavimba na alikuwa hapati dawa wala huduma yoyote ya matibabu anayohitaji nchini Venezuela.”

Mwishoni mwa mwaka 2018, mamlaka za mji wa Maicao na serikali ya Colombia ziliimboa UNHCR msaada wa kuweka kituo cha mapokezi ya muda kusaidia kushughulikia upungufu wa makazi kwa watu wengi wenye uhitaji.

Mkuu wa ofisi ya UNHCR iliyoko La Guajira, Bwana Federico Sersale anasema,

(Sauti ya Federico Sersale)

“Lengo la kituo hiki ni kutoa suluhisho la muda mfupi kwa mazingira hatarishi ambayo watu wanakabiliana nayo, kisha baadaye itawasaidia kuchangamana na jamii wenyeji.”

Kutokana na huduma hii, hivi sasa familia 60 zimeshapata nafuu ya maisha ingawa  UNHCR inasema bado mahitaji ni makubwa kwa wavenezuela zaidi ya milioni 3.5 walioko nje ya nchi yao wakisaka usalama na mstakabali wa maisha yao.

Audio Credit
John Kibego
Sauti
1'36"
Photo Credit
UNHCR/Stephen Ferry