Teknolojia za watu wa asili kumulikwa wakati wa jukwaa lao New York

22 Aprili 2019

Mkutano wa jukwaa la kudumu kuhusu masuala ya watu wa asili unaanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ukileta pamoja zaidi ya watu 1,000 wa  jamii ya watu asili kutoka kona mbalimbali duniani.

Dkt. Elifuraha Laltaika, ambaye amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa jopo la wataalamu huru wa jukwaa hilo akiwasilisha Afrika tayari yuko New York Marekani na amezungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na hapa anafafanua kwa kina kile watakachoangazia akisema, “mwaka huu tunajikita katika maarifa ya asili. Na katika kuchakata maarifa ya asili tunaangazia namna ambavyo yanawasilishwa na kurithishwa kwa kizazi kimoja hadi kingine. Na ukingalia hiyo ni muhimu sana kwasababu mwaka huu Umoja wa Mataifa umeamua uwe mwaka wa lugha za asili na sisi tunaamini kwamba maarifa ya asili yanategemea sana uelewa wa zile lugha za asili kama moja  ya namna ya kurithisha lakini pia ya kuwasilisha yale maarifa ya asili,”

Alipoulizwa ni kwa nini  basi wamejikita kwenye teknolojia za asili, Dkt. Laltaika amesema, “tunaangalia sasa teknolojia itaboreshwa namna gani ili isiathiri maarifa ya asili lakini iongeze thamani au ladha katika kurithisha maarifa hayo. Kwa hiyo ni kitu cha muhimu sana kuangalia je teknolojia itaathiri au itaboresha maarifa ya asili na tangu mwaka jana tulishaamua kuwa mustakabali wa jamii unategemea sana, nyanja tofauti tofauti ikiwemo pia ya  uvumbuzi hata ya madawa na kadhalika na kadhalika.

Kando mwa maudhui hayo makuu, jukwaa hilo pia litajadili mwaka huu wa 2019 ambao ni mwaka wa kimataifa wa watu wa asili sambamba na ajenda ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa haki za watu wa jamii ya asili.

Audio Credit:
Arnold Kayanda/Elifuraha Laltaika
Audio Duration:
1'55"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud