Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya teknolojia yahatarisha afya ya wafanyakazi duniani- ILO

Maendeleo ya teknolojia yahatarisha afya ya wafanyakazi duniani- ILO

Pakua

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani ILO inasema kila siku watu 7500 hufariki dunia kutokana na mazingira yasiyo salama na afya kazini. Arnold Kayanda na maelezo zaidi.

Mabadiliko ya mazingira ya kazi, teknolojia za kisasa na kitendo cha mtu kuweza kufanya kazi popote pale alipo na wakati wowote pamoja na ukosefu wa usalama kazini ni sehemu tu ya mambo yanayosababisha vifo hivyo kila uchao kote duniani.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina usalama na afya kama kitovu cha mustakabali wa  kazi, kujenga kutokana na uzoefu wa miaka 100 ya ILO, inasema kando ya idadi hiyo, kila mwaka watu zaidi ya milioni 374 wanajeruhiwa au wanaugua kutokana na ajali kazini ikiwemo kufanya kazi muda mrefu.

Manal Azzi, ni mtaalamu wa ILO kuhusu usalama kazini anasema labda uwe umelala lakini, “watu mbalimbali wanafanya kazi kwa njia mbalimbali ikiwemo simu, kompyuta mpakato unazoweza kwenda nazo kila pahali. Intaneti inapatikana kwa kila mtu, simu za kimataifa zinafanya mtu aweze kupatikana wakati wowote.”

 Manal anasema katika mazingira hayo wafanyakazi wanatakiwa kufanya  kazi zaidi na zaidi na hawana muda wa kupumzika hali inayoweza kusababisha magonjwa ya akili, msongo wa mawazo na hata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani na moyo.

ILO inapendekeza mambo sita ikiwemo será bunifu za za ajira zinazojali afya ya umma na kuimarisha sheria za viwango vya kazi kimataifa na kitaifa.

 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Arnold Kayanda
Audio Duration
1'29"
Photo Credit
ILO