Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kliniki  ya macho Beni nchini DRC yasaidia manusura wa Ebola

Kliniki  ya macho Beni nchini DRC yasaidia manusura wa Ebola

Pakua

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Congo, DRC shirika la afya ulimwenguni WHO kwa kushirikiana na Wizara ya afya pamoja na vyuo vikuu viwili kutoka Marekani wanasaidia manusura wa Ebola kujiepusha na ugonjwa wa macho.  

Mjini Beni kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kliniki na macho inaendelea kwa manusura wa ugonjwa wa Ebola.

Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, WHO na vyuo vikuu viwili kutoka Marekani wanachunguza macho ya wagonjwa waliopona Ebola kwani uzoefu wa Ebola huko Afrika Magharibi ulibaini kuwa wako hatarini kupata uoni hafifu utokanao na kuwepo kwa uvimbeuchungu ndani  kwenye macho.

Kliniki hii ina vifaa vya kisasa na inaongeza nguvu ya kliniki ya kila mwezi zilizoko Beni, Mangina na Butembo ambazo zilianzishwa mwezi Novemba mwaka jana kufuatia mlipuko wa Ebola ulioanza mwezi Agosti.

Dokta Jessica Shantha kutoka Chuo Kikuu Emory nchini Marekani anasema,

(Sauti ya Dokta Jessica Shantha)

“Tunawachunguza wagonjwa mapema zaidi kuliko tulivyofanya awali. Inawezekana kuwa hawajapata huu ugonjwa. Kwa hiyo ni jambo ambalo wanapaswa kufuatiliwa kwa muda mrefu ili kuhakikikisha hawapati tatizo au uvimbeuchungu kwenye macho. Na pia nadhani sote bado tunajifunza kutoka kwa manusura wa Ebola, ugonjwa wa macho na matatizo ya macho.”

Madaktari hawa wa kimataifa wanasaidia pia madaktari wa DRC kufahamu vyema jinsi ya kuchungua na miongoni mwao ni Dkt. Telesphore Mumbere.

(Dkt. Telesphore Mumbere)

“Kwa ushirikiano na WHO tunapaswa kuwaona hawa wagonjwa kila mwezi ili kutathmini waliopatiwa tiba kama wanapata nafuu na kwa wengine kuona iwapo wamepata tatizo zaidi kama ambavyo tumeshuhudia leo hii.”

Manusura wa Ebola anayepata tiba kwenye kituo hiki ni Centrine na anasema,

(Sauti ya Centrine)

Niliweza kuona kuwa walikuwepo pale kutupatia matibabu. Sikuhofia, nilielewa kuwa wanatibu macho yetu. Walikuwepo watu wengi wakiwemo wazungu.”

Hivi sasa kuna manusura zaidi ya 300 wa Ebola ambao wamejisajili kupata matibabu ya macho.

 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'49"
Photo Credit
J.D.Kannah/WHO