Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za UNHCR nchini Côte d’Ivoire zanusuru watoto wasiokuwa na utaifa

Harakati za UNHCR nchini Côte d’Ivoire zanusuru watoto wasiokuwa na utaifa

Pakua

Nchini Côte d’Ivoire, kampeni kabambe iliyoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na watetezi wa haki kuhusu haki ya mtu kupata utaifa imezaa matundana kuleta nuru kwa wasichana wawili ambao tangu kuzaliwa hadi kutimiza umri wa miaka 17 nchini humo hawakuwa na utaifa.

Ndani ya kituo cha watoto yatima kikipatiwa jina Nest au Kiota, kwenye mji wa Korogho, nchini Côte d’Ivoire, wasichana wawili Christelle Karidja Camara na Françoise Yeo Pandjawa wanaandaa mlo kwa ajili yao na watoto wengine yatima.

Wawili hawa wenye umri wa miaka 17 walifikishwa hapa baada ya mama zao kufariki dunia punde tu baada ya kuzaliwa na baba zao kuwakana, hali iliyosababisha washindwe kupata utaifa.

Nchini Côte d’Ivoire ni lazima angalau mzazi mmoja awe mzawa.

Hata hivyo  harakati za shirika la  Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR pamoja na wadau wake zimefanikisha mahakama nchini Côte d’Ivoire kupitisha uamuzi wa Christelle na Françoise kupatiwa uraia na afisa wa shirika hilo Layse Farias anasema..

(Sauti ya Layse Farias)

Hii inaweka mazingira ya utambulisho wa kisheria kwa watoto hawa. Sasa wanaweza kufanya tukio lolote la kiraia kwenye maisha yao ikiwemo ndoa, kumaliza masomo yao hadi Chuo Kikuu na kupata ajira rasmi. Si hivyo tu, kwa wao inamaanisha pia kujumuishwa kwenye  taifa.”

Sasa Christelle na Françoise wamekabidhiwa vyeti vyao vya utambulisho na wanarejea kituoni kwao wakiwa na amani, furaha na matumaini.

Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'30"
Photo Credit
UN OCHA/GILES CLARKE