Restless Development yazidi kuchagiza jamii kuhusu madhara ya ukatili wa jinsia
Ukatili wa jinsia ni suala ambalo limekuwa kikwazo kwa maendeleo ya jamii hasa kwenye maeneo ambako mfumo dume umeshamiri na wanawake wanakumbwa na ukatili huo katika njia mbalimbali. Umoja wa Mataifa unatambua kuwa ukatili wa jinsia ni kikwazo na ndio maana unapigia chepuo usawa wa jinsi na kutokomeza mila potofu na hata sheria ambazo kwa njia moja au nyingine zinashamirisha ukatili wa jinsia. Hata hivyo changamoto ni pale ambapo jamii inakuwa ina uoga au hata pengine hawatambua kuwa kitendo fulani ni ukatili wa jinsia. Ni kwa kuzingatia hilo shirika la kiraia la Restless Development lina vijana waleta mabadiliko ambao wanapita mashinani kuelimisha umma kuhusu ukatili wa jinsia na miongoni mwao ni Thobias Komba ambaye anatoka Dodoma mkoani Tanzania na hivi sasa yuko jijini New York, Marekani akihudhuria mkutano wa 63 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW. Assumpta Massoi amezungumza naye na kumuuliza pamoja na mambo mengine hatua ambazo wanachukua kuelimisha umma kuhusu ukatili wa jinsia zinazaa matunda na je jamii inaitikia?