Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Barani Afrika bado wanawake na wasichana wanakabiliwa na vikwazo lukuki, tubadilike- UNESCO

Barani Afrika bado wanawake na wasichana wanakabiliwa na vikwazo lukuki, tubadilike- UNESCO

Pakua

Ukatili wa kijinsia, uwakilishi mdogo katika uongozi wa tasnia ya habari na kutowezeshwa kujimudu kiuchumi ni moja ya changamoto zinazoendelea kuwakabili wanawake wengi barani Afrika ikiwemo nchini Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO nchini Tanzania Tirso Dos Santos katika ujumbe wake kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo kila mwaka hufanyika Machi 8.

Bwana. Dos santos amesema kwa kulitambua hilo mathalani nchini Tanzania UNESCO imejitoa kimasomaso kupigia upatu haki za binadamu, kuwalinda wanawake na kuchagiza mchango wao katika jamii kwani hata katika zama hizi za utandawazi na kidijitali wanawake bado wanaachwa nyuma , hivyo amesema

“Hususan ofisi yangu imeweka mipango ya kushughulikia mila potofu zinazowakandamiza wanawake katika jamii hasa ukatili wa kijinsia ambao ni suala moja linalotia hofu.”

Kwa wasichana na  vijana amesema

“Hivi karibuni tumezindiua program ya Afrika nzima tunaiita programu hiyo maisha yetu, haki zetu na mustakabali wetu, na inalenga kuwapa wasichana na vijana elimu kuhusu ngono ili waweze kukabiliana vyema na hali yao katika jamii.”

Na hata katika tasnia ya habari anasema

“Wanawake bado wako nyuma katika ushiriki , tunaona jamii ambayo wanaume ndio waliotawala vyombo vya habari suala ambalo linahitaji kupatiwa uwiano.”

Sasa suluhu ni ipi?

“Ni muhimu kujikita kushughulikia suala la ukatili dhidi ya wanawake wanahabari kwa kuchagiza ushiriki wao katika ngazi zote za mitazamo ya habari ikiwemo uongozi wa vyombo vya habari”

Audio Credit
Arnold Kayanda/Flora Nducha
Audio Duration
1'54"
Photo Credit
UN /Rick Bajornas