Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa chakula Zemio, CAR kufikishwa kwa njia ya anga-WFP

Msaada wa chakula Zemio, CAR kufikishwa kwa njia ya anga-WFP

Pakua

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP hii leo limetangaza kuzindua operesheni ya kusafirisha chakula kwa kutumia ndege ili kuokoa maisha ya watu 18,000 katika eneo la Zemio takribani kilomita 1000 mashariki mwa mji mkuu wa Afrika ya kati, Bangui. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na WFP, eneo hilo liko katika hatari ya baa la njaa na ukosefu wa lishe kwasababu ya mchanganyiko wa masuala kadhaa kama vile ukosefu wa usalama na changamoto za miundombinu ambavyo vinaathiri uwezekano wa watoa misaada kufika huko.

Mkuu wa WFP nchini Afrika ya kati Gian Carlo Cirri anasema hali ya kibinadamu katika eneo la Zemio ni ya hatari inaweza kubadilika haraka na kuwa janga ikiwa hawatachukua hatua hivi sasa.

Amesema wadau wao walioko huko wanasema wanawake na watoto hawana chakula cha kutosha na watu wanaishi katika hali mbaya sana.

WFP itawapatia chakula wakimbizi wa ndani na wenyeji ambao wamekuwa wakiwatunza wakimbizi hao. Chakula maalumu cha lishe kitasambazwa katika familia zenye watoto wadogo, wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha.

Kwa kawaida WFP huwa inasafirisha misaada kuelekea Zemio kupitia Obo kwa njia ya barabara kutoka nchi jirani ya Uganda na baadaye kwa njia ya maji ya mto kutoka katika mji mkuu Bangui kupitia Bangassou, lakini kutokana na kuvunjika kwa daraja na kivuko kisichofanya kazi kwa sasa nji hizo zimeshindikana na sasa wanatumia  njia ya anga.

Herve Verhoosel msemaji wa WFP huko Geneva, Uswisi anafafanua hatua ya kusafirisha chakula kwa ndege.

“Ni wazi kuwa ni gharama kubwa kusafirisha chakula kwa njia ya  ndege na si kukidondosha kutoka angani. Ina maana ndege zinatua na chakula kikifika kuna watu wa kusambaza. Tunakadiria ni muhimu ingawa na gharama kufanya operesheni hii kwa sababu hali huko Zemio ni mbaya hivi sasa na si rahisi kufika kwa gari. Tutasitisha usafirishaji kwa ndege baadaye wiki hii na kutathmini upya hali ilivyo kulingana na hali ilivyo ya usafirishaji kwa njia ya barabara na pia hali ya usalama Zemio.”

Mgogoro wa muda mrefu umewaathiri watu takribani milioni 2.1 wa C.A.R ambao ni takribani nusu ya watu wote nchi nzima.

Katika mwaka huu wa 2019 WFP inahitaji dola za kimarekani milioni 87 kuweza kumudu kutoa msaada wa kuokoa maisha kupitia katika misaada ya vyakula, fedha, na program za lishe kwa angalau watu milioni 1.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Grace Kaneiya
Audio Duration
2'36"
Photo Credit
UNICEF/Peter Martell