Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Narudi nyumbani Burundi kwa kuwa amani imerejea- Mkimbizi

Narudi nyumbani Burundi kwa kuwa amani imerejea- Mkimbizi

Pakua

Kufuatia kuimarika kwa hali ya usalama nchini Burundi, raia wa nchi hiyo ambao walisaka hifadhi ugenini wanaendelea na mipango ya kurejea nyumbani ili hatimaye waweze kujenga nchi yao huku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR likisaka dola milioni milioni 296 kusaidia wakimbizi waliosaka hifadhi nchi jirani kwa mwaka huu wa 2019. John Kibego na maelezo zaidi.

Ni kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya, kimbilio la Alexis Rukundo, raia kutoka Burundi na wasaka hifadhi wengine 13,000 kutoka nchi hiyo ya Maziwa Makuu.

Alex mwenye umri wa miaka 29 na mkewe na watoto wao wawili wameishi kwenye kambi hii kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu lakini sasa mke wake na wanae wanafungasha virago tayari kurejea nyumbani ili kujenga maisha yao.

 “Nilikimbia Burundi kwasababu ya ghasia. Nilitaka kuwepo kwenye nchi ambayo ina amani. Nimekuwepo hapa Kalobeiyei kwa mwaka mmoja na nusu. Sasa nimesikia nyumbani kuna amani. Kile ambacho nilikimbia, sasa hakipo. Nimeieleza familia yangu kuwa kuna amani na tumeamua kurejea.”

Rukundo alinufaika na sera za ujumuishi wa wakimbizi kwenye makazi ya Kalobeiyei yaliyoko kambini Kakuma ambapo alikuwa anaendesha biashara ya usafirishaji.  

Hapa wakimbizi wanahamasishwa kujumuisha kiuchumi na kijamii na jamii za wenyeji na hivyo alikuwa anafanya biashara ya kusafirisha abiria kwa pikipiki au bodaboda.

“Nimefanya kazi na nimetunza kiasi cha fedha. Nitakapofika Burundi, nataka kuanza maisha ya kufanya biashara.”

Rokundo na familia  yake walikuwa miongoni mwa kundi la wakimbizi 280 ambao wameondoka makazi ya Kalobeiyei na kurejea Burundi kupitia mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake limezindua ombi maalum la kufadhili na kusaidia wakimbizi wa Burundi pamoja na nchi zinazowahifadhi kwa kuzingatia kuwa ufadhili wa mpango huo huchangiwa kwa kiasi kidogo.

Audio Credit
Assumpta Massoi/ John Kibego
Audio Duration
2'4"
Photo Credit
UNHCR/Georgina Goodwin