Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwendesha mashtaka ICC ashindwa kuthibitisha makosa dhidi ya Rais wa zamani wa Côte d'Ivoire!

Mwendesha mashtaka ICC ashindwa kuthibitisha makosa dhidi ya Rais wa zamani wa Côte d'Ivoire!

Pakua

Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC leo imemwachia huru rais wa zamani wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo na aliyekuwa mkuu wa tawi la vijana Charles Blé Goudé baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasipo shaka mashtaka yote dhidi yao. 

Wawili hao, Gbagbo na Blé Goudé walikuwa wanatuhumiwa kuhusika na makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo ubakaji  na mauaji ambayo yanadaiwa kutendwa nchini Côte d'Ivoire mwaka 2010 na 2011 baada ya uchaguzi wa rais.

Majaji watatu walikuwa wanaendesha kesi hiyo ambapo wawili wao Jaji Cuno Tarfusser ambaye alikuwa kiongozi,  na Jaji Geoffrey Henderson walisema hakuna kesi ya kujibu ilhali jaji Herrera Carbuccia hakuwa na makubaliano yoyote.

Majaji hao wawili wametambua uwepo wa ghasia za kisiasa baada ya uchaguzi wa rais mwaka 2010 huko Abidjan na kwingineko lakini wamesema kuwa mwendesha mashtaka ameshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Gbagbo na Blé Goudé walitekeleza makossa yaliyokuwa yanawakabili. Hivyo Jaji Tarfusser amesema..

 “Mahakama baada ya kuchambua kwa kina ushahidi wote na kuzingatia hoja zote za kisheria kwa maneno na maandishi kutoka pande zote imebaini kuwa hakuna sababu ya upande wa utetezi kuwasilisha ushahidi zaidi kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuhusiana na mashtaka husika. Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwepo mpango wa pamoja wa kumweka madarakani Gbagbo ikiwemo mpango wa mauaji dhidi ya raia.”

Mahakama imeagiza Gbagbo na Blé Goudé waachiliwe huru na kwamba mwendesha mashtaka anaweza kuomba waendelee kusalia rumande kwa sababu maalum na zaidi ya yote anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Arnold Kayanda
Sauti
1'49"
Photo Credit
ICC