Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tshisekedi asema atakuwa rais wa wote DRC

Tshisekedi asema atakuwa rais wa wote DRC

Pakua

Kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya  uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo Felix Tshisekedi ameibuka mshindi, Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa amepongeza wananchi wa DRC na Tume ya huru ya taifa ya uchaguzi kwa mwenendo mzima wa uchaguzi. 

Sauti hiyo ya Corneille Nangaa, Rais wa tume huru ya taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati akitangaza jana jumatano matokeo ya uchaguzi wa rais  uliofanyika nchini humo tarehe 30 mwezi uliopita.

Matokeo ni kwamba Felix  Tshisekedi Tshilombo wa chama cha UDPS  amepata asilimia 38.57 ya kura zote zilizopigwa, akizidi wenzake kwa zaidi ya kura milioni 7.

Mgombea  Martin Fayulu Madidi kutoka muungano wa vyama vya upinzani aliyepata asilimia  34.83 ilhali Emmanuel Ramazani kutoka chama tawala akipata asilimia 23.84.

Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo ambayo yanasubiri kuidhinishwa na mahakama ya kikatiba, rais mteule Tshisekedi ameshukuru wananchi wa DRC akisema kuwa..

« Mimi sitakuwa rais wa chama cha kisiasa cha UDPS bali nitakuwa rais wa wanawake na wanaume wote wa DR Congo. »

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa taarifa kupitia msemaji wake jijini New York, Marekani ya kutambua taarifa hizo na amepongeza wananchi wa DRC na wanasiasa kwa vile waliendesha na kushiriki uchaguzi huo wa rais, majimbo na wabunge kwa kutoa fursa jumuishi ya ushiriki.

Ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na ghasia zozote na kuwasilisha malalamiko yoyote ya mchakato huo kwenye mifumo iliyowekwa kwa mujibu wa katiba ya DRC na sheria nyingine husika za uchaguzi.

Halikadhalika amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea na ushirikiano na wadau wa kikanda na wale wa kimataifa katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo nchini DRC.

Hata hivyo wilaya tano nchini DRC hazikushiriki kwenye uchaguzi huu mkuu kutokana na sababu za kiusalama na ugonjwa wa ebola.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi iliyotolewa mwaka jana, Rais mteule anatarajiwa kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
MONUSCO/John Bopengo