Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikosi vya MINUSMA ni zaidi ya ulinzi vijijini Mali

Vikosi vya MINUSMA ni zaidi ya ulinzi vijijini Mali

Pakua

Tangu kupitishwa kwa azimio la kuongeza muda kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA na Baraza la Usalama la Umoja huo, kazi ya kulinda raia na mali zao zimepelekwa hadi katikati mwa Mali katika maeneo ambako ni vigumu kuyafikia ikiwemo vijijini.

Ni ndege ikitua, katika kijiji cha Dangatene nchini Mali ambacho kinajumuisha nyumba chache zilizojengwa kwa udongo.Ni hali ya mgeni njoo mwenyeji apone kwa wanakijiji ambao wamepanga foleni wakisubiri wageni wao kwa ajili ya kupokea matibabu.

MINUSMA inasema imeweza kutibu takriban watu 200 katika kijiji hicho, kazi ambayo wanasema inahitaji kujitolea na zaidi ya yote, uvumilivu. Luteni Tafsir Gueye ni afisa wa afya kutoka kikosi cha Senegal.

(Sauti ya Gueye)

Tuko hapa kama wafanyakazi wa kujitolea na wa misaada ya kibinadamu kusaidia wakazi wa mashinani kukabiliana na mahitaji yao ya kimsingi ya afya. Kwa sababu hatuna vifaa vyote ambavyo tunahitaji, tunafanya kila tuwezalo kukabiliana na hali ya sasa.”

Ujio wa vikosi hivyo umeleta furaha kwa wanakijiji ikiwemo Kouny Weme mwanamke mwenye umri wa miaka 62.

(Sauti ya Weme)

“Baada ya kuchunguzwa, nimeandikiwa dawa na kupewa, ninafuraha sana baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari, nimejiskia nafuu baada ya ushauri wa daktari, amefanya kazi nzuri.”

Mzozo ulioanza mwaka 2012 nchini Mali ulisababisha watu wengi kufurushwa makwao na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wakazi wa eneo la katikati mwa nchi hiyo.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'39"
Photo Credit
Marco Dormino