Nilikuwa na hofu ugenini, lakini sera za Rwanda zimeniondoa uhofu- Mhamiaji

28 Disemba 2018

Mpango wa kujumuisha wakimbizi katika maendeleo ya kiuchumi kwenye mji mkuu wa Rwanda, Kigali, umechangia katika wakimbizi kuanzisha biashara ndogo ndogo ambazo zimebuni ajira kwa watu 2,600 nchini humo, ikiwemo biashara ya kuuza mitungi ya gesi inayomilikiwa na mkimbizi kutoka Burundi. Taarifa zaidi na  Ramadhani Kibuga.

Hiyo ni sauti ya Annick Iriwacu mkimbizi kutoka Burundi akiwa kwenye duka lake la kuuza mitungi ya gesi.

Annick alikimbilia Rwanda mwaka 2015 ambapo anasema ujio wake na familia ulikabiliwa na changamoto nyingi mwanzoni kwani hali ilikuwa ngumu baada ya kujikuta ukimbizini lakini kwa kuwa alizoea kujitegemea aligundua kuwa kuwepo Kigali, mji unaotajwa kuwa mji safi zaidi Afrika ilikuwa ni fursa ya biashara.

“Nilianzaisha biashara ya kuuza mitungi ya gesi kwa sababu niligundua kuwa maono ya Rwanda ni kuwa mji safi na unaojali mazingira, mtaji ulikuwa mkubwa lakini nilikata kauli kuanzisha biashara hiyo.”

Baada ya maamuzi yake Annick alipata mkopo kwa sababu wakimbizi wanaruhusiwa kuomba mikopo na wanalipa ushuru kwa hivyo.

“Faida ya kuwepo Kigali ni kwamba unaweza kufanya kazi, unaweza kufanya kazi kwa mikono yako na kutangaza biashara yako.”

Serikali ya Rwanda kwa ushirikiano na sekta binafsi wanasaidia wakimbizi kuanzisha biashara. Lydia Irambona ni Mkurugenzi wa programu ya wakimbizi katika kampuni binafsi ya kutoa ushauri ya Inkomoko.

"Ni lazima kuwe na utashi wa kisiasa, nchini Rwanda imekuwa rahisi kwa sababu nchi ilitia saini kuwajumuisha wakimbizi katika ukuaji wa kiuchumi na kwa sekta binafsi. Hii ni hali ya ushindi kwa pande zote kwa sababu wakimbizi huja na stadi, ujuzi na utamaduni tofauti ambavyo huenda ni mchango muhimu.”

Kufikia sasa Inkomoko imewawezesha wakimbizi 809 kuanzisha biashara, ambapo wamebuni nafasi 2,600 za ajira na kuwawezesha kuchangia katika jamii zilizowakaribisha.

Audio Credit:
Siraj Kalyango/ Ramadhani Kibuga
Audio Duration:
2'15"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud