Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za Rebeca Gyumi za kumkomboa mtoto wa kike Tanzania zatambuliwa UN

Harakati za Rebeca Gyumi za kumkomboa mtoto wa kike Tanzania zatambuliwa UN

Pakua

Washindi wa tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa  Mataifa kwa mwaka 2018 hii leo wamepatiwa tuzo hizo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani.

Washindi hao ambao ni watu watatu na shirika moja, wamekabidhiwa tuzo hizo wakati wa kikao cha 58 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichoongozwa na Rais wa Baraza hilo Maria Fernanda Espinosa.

Bi.Espinosa ndiye amefungua kikao hicho ambapo kabla ya kukabidhi zawadi amezungumza na kusema kuwa washindi wote wamejikita katika haki za binadamu kuanzia za wanawake, wahamiaji, na a zaidi ya yote..

“Tuzo hii pia ni ujumbe wa shukrani kwa watetezi wote wa haki za binadamu popote pale walipo, kwasababu kujitoa kwao na kuendelea kupambana kumetuwezesha kuwa na jamii ambayo angalau pengo la kutokuwepo usawa na haki si kubwa. Na kwa washindi wa leo tunaelezea mshikamano nao, na kwamba jitihada zao ni ushahidi kuwa vitendo ni muhimu na kila wakati tunaweza kuleta mabadiliko.”

Kisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akasema kuwa mara nyingi kazi za watetezi wa haki za binadamu ni za hatari wakikumbwa na mauaji, mateso, kutoweshwa na hata kufungwa lakini washindi wamekuwa jasiri akisema..

“Napenda kutoa pongezi kwa Rebeca Gyumi kutoka Tanzania, mwanaharakati wa haki ya elimu kwa wasichana; kwa hayati Asma Jahangir, kutoka Pakistan; kwa Joênia Batista de Carvalho, mwanamke wa kwanza wa jamii ya watu wa asili kuwa mwanasheria; na kwa shirika la Front Line Defenders kutoka Ireland, kwa kufanya kazi kulinda watetezi wa  haki walio hatarini. Kazi zao na zile za watetezi wa haki za binadamu kote duniani ni muhimu kwa jukumu letu la pamoja la kusongesha amani na kuhakikisha maendeleo jumuishi endelevu na heshima ya haki za binadamu kwa wote.”

Na ndipo muda wa tuzo ukawadia…

Tukio hili lilifuatiwa na kikao maalum kwa washindi kuzungumza na kujibu hoja kutoka kwa washiriki ambapo Rebeca Gyumi amesema leo ni wakati wa kujivunia siyo tu yeye bali pia nchi yake Tanzania na jamii yake na kwamba

“Nahisi kama huu ni ushuhuda kuwa wasichana popote pale walipo; unaweza na mnaweza kuwa chochote kile bila kikwazo, na ni jambo ambalo tumekuwa tunapigania kuweka mazingira ambamo kwayo mtoto wa kike anaweza kuchanua bila kuwa na hofu kuwa siku ijayo mzazi anaweza kuibuka na kukueleza kuwa tumekupatia mume.”

Amesema dunia ambayo mtoto wa kike anaweza kuota ndoto na kufikia bila kikwazo, ndio dunia ambayo yeyé na taasisi aliyoanzisha ya Msichana Intiative ndiyo wanahaha kuifikia Tanzania.

 Washindi wa tuzo hii walitangazwa mwezi uliopita wa Novemba.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
3'12"
Photo Credit
UN / Evan Schneider