Huduma za afya zisibague, kila mtu anastahili popote pale alipo

12 Disemba 2018

Leo ni siku ya kimataifa ya huduma za afya kwa wote duniani ambapo Umoja wa Mataifa unasema afya bora ni haki ya msingi ya binadamu na kiungo muhimu cha kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu yaani SDGs ifikapo mwaka wa 2030. 

Kilio cha mtoto, kiashiria cha uhai punde tu baada ya kuzaliwa! Mustakabali wa mtoto huyu unategemea huduma ya afya si kwake yeyé tu bali pia mzazi wake.

Ni kwa kuzingatia hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika ujumbe wake wa maadhimisho haya ya kwanza ya siku ya kimataifa ya huduma za afya kwa wote yenye kauli mbiu ya tuungane kwa huduma  ya afya kwa wote na wakati wa kuchukua hatua ni sasa, amesema kuwa,uongozi imara na pia kuhusisha jamii ni muhimu kuhakikisha kuwa  watu wote wanapata huduma bora  wanazohitaji kuhusu afya zao na popote pale walipo.

Mathalani katika makazi ya wakimbizi ya Mantapala nchini Zambia yanayohifadhi raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, huduma za afya ya mama na mtoto zinapatikana bila kujali mtu ni mkimbizi au mwenyeji kama anavyoelezea muuguzi Patricia Sampule aliyesaidia mjamzito mkimbizi kujifungua mtoto.

“Mtoto yu salama, halikadhalika mama mtoto, kila kitu kiko sawa.”

Huduma hizi zinatolewa katika kituo cha afya kinachohudumia wakimbizi na wenyeji ambapo Abdon Mwere, kamishna wa wakimbizi nchini Zambia anasema..

“Ni muhimu miradi ya wakimbizi inufaishe pia wenyeji wanaowahifadhi. Hivyo unaona kupitia mfumo huu hapa Mantapala, huduma tulizoweka, tumeziweka kwenye jamii ambako wakimbizi 24 wamesaka hifadhi.”

Audio Credit:
Flora Nducha/Arnold Kayanda
Audio Duration:
1'48"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud