Gharama za kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni ndogo zikilinganishwa na faida zake kiafya.

5 Disemba 2018

Kuyafikia malengo ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi kunaweza kuokoa maisha ya takribani watu milioni moja kwa mwaka duniani kote ifikapo mwaka 2050 kupitia kupunguza uchafuzi wa hewa pekee.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la afya duniani, WHO iliyozinduliwa leo wakati wa mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 huko Katowice, Poland, ikieleza kwa nini masuala ya afya ni muhimu katika kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na huku ikitoa mapendekezo muhimu kwa watunga sera.

Ripoti hiyo inafafanua kwa kina kuwa, uchafuzi wa hali ya hewa unasababisha vifo milioni 7 duniani kote kila mwaka na kugharimu takribani dola trilioni 5.11 hasara duniani kote.

Katika nchi 15 ambazo zinazalisha hewa chafu, athari mbaya za hali ya hewa kwa afya inakadiriwa kugharimu zaidi ya asilimia 4 ya pato lao kwa mwaka  ilihali hatua za kufikia malengo ya Paris kutagharimu takribani asilimia 1 ya pato katika nchi hizo.

Mkurugenzi  Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema, “mkataba wa Paris ni mkataba muhimu sana kwa upande wa afya katika karne hii. Ushahidi uko wazi kuwa mabadiliko ya tabia nchi tayari yamesababisha matatizo makubwa kwa afya na maisha ya binadamu. Inatishia kila tunachokihitaji kwa ajili ya afya bora kama vile hewa safi, maji safi ya kunywa, chakula chenye lishe na malazi bora. Hatuwezi kumudu kuendelea kuchewa zaidi”

Dkt Maria Neira mkurugenzi wa WHO akihusika na idara ya afya ya umma, mazingira na jamii anasema, “gharama ya kweli ya mabadiliko ya tabianchi inaweza kuhisiwa katika hospitali zetu na mapafu yetu.”

Ripoti hiyo ya WHO kuhusu mabadiliko ya tabianchi imetoa mapendekezo ambayo ni pamoja na kutambua na kuhamasisha matendo ambayo yanaondoa uzalishaji wa hewa ya ukaa na kupunguza pia uchafuzi wa hewa.

Halikadhalika kuhakikisha kuwa ahadi za kulinda afya zilizofikiwa katika mkataba wa kimataifa wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC na mkataba wa Paris zinaonekana kwa ngazi ya kitaifa na kidunia. Pia kuondoa vikwazo kwa uwekezaji katika mabadiliko yanayolenga kulinda afya katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kujikita katika mifumo sitahimilivu ya kiafya.

Audio Credit:
Flora Nducha
Audio Duration:
2'18"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud