Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpira utamwepusha kijana kwenda kubeba bunduki- Mutombo

Mpira utamwepusha kijana kwenda kubeba bunduki- Mutombo

Pakua

Balozi wa kimataifa wa chama cha mpira wa kikapu nchini Marekani,  NBA, Dikembe Mutombo amesema kuwapatia vijana elimu inayowawezesha kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani ni suala mujarabu katika kutekeleza lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs linalohusu amani, haki na taasisi thabiti.

Bwana Mutombo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amesema hayo alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili  ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kushiriki mkutano ulioandaliwa na Qatar na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC ukiangazia mpango wa elimu kuhusu haki, E4J.

Mcheza mpira huyo wa kikapu mashuhuri ambaye sasa amestaafu akasema kufanikisha Elimu kuhusu haki kuna mengi ya kufanya…

“Elimu bado ni ufunguo wa mafanikio, lakibni michezo nayo ina dhima yake. Iwapo utawarushia mpira wa kucheza vijana wetu wanapotoka darasani saa saba, unaweza kuweka mawazo yao na jambo la kufanya kabla ya kufanya kazi za shule. Wanaweza kufirikia kushinda mchezo, mazoezi na kuwa na marafiki zao  badala ya kubeba bunduki na silaha na kwenda kufanya mambo mabaya.”

Alipoulizwa ujumbe wake kwa vijana, Mutombo ambaye anaongoza taasisi ya Mutombo huko nchini mwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amesema..

“Mustakhbali wa dunia yetu uko mikononi mwao. Sisi ambao tumekuja kabla yao tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu ili kuandaa dunia hii tuyyolipewa ili iwe pahala bora kwa kizazi kijacho. Ni lazima wafuate utawala wa sheria na kuheshimu sheria ambazo zimekuwa zinatumika kwenye bara hili na ulimwenguni.

Audio Credit
Grace Kaneiya/Arnold Kayanda
Sauti
1'52"
Photo Credit
UN Photo.