Visa vya ukatili wa kingono sasa vyashughulikiwa kwa haraka- Lacroix akizungumzia manufaa ya A4P

25 Septemba 2018

Mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukianza leo, wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wa nchi zinazochangia kwenye operesheni za ulinzi wa amani wanakutana kujadili jinsi ya kukabiliana na changamoto za ulinzi wa amani na kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza kampeni ya hatua za pamoja kwa ajili ya ulinzi wa amani. Anold Kayanda na taarifa kamili.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix [Larkwa] amesema mafanikio ni pamoja na kupunguza muda wa kuchukua hatua pindi mlinda amani anapokabiliwa na tuhuma za ukatili wa kingono.

Nadhani sasa tuko vizuri zaidi kuliko awali. Tumeongeza msaada kwa manusura, tumepunguza pia muda tangu tuhuma zinapoibuka na nchi ambako mliinda amani anatoka inachukua hatua. Lakini tunapaswa kuchukua hatua zaidi. »

Suala lingine ni usawa wa kijinsia katika ulinzi wa amani ambapo Bwana Lacroix anaelezea kile kinachopaswa kufanya kuondoa hali ya sasa..

Nadhani kuna vitu vingi tunavyoweza kufanya, na ni shabaha muhimu sana kwa sababu, kukiwa na wanawake wengi katika ulinzi wa amani ina maana kuwa ulinzi unakuwa madhubuti. Kwa hiyo mosi ni kuwaomba wanachama kuwa waendelee kufanya juhudi hizo za kutupatia idadi kubwa zaidi ya walinda amani wanawake. Pili ni kuhakikisha kuwa mazingira yetu ya kazi ni sahihi kwa wanawake. Nadhani ya tatu ni kuona kama tunatoa mwanya zaidi kwa wanawake kuweza kuchagia zaidi katika ulinzi wa amani.”

 

Mkakati wa hatua za pamoja kwa ajili ya  ulinzi  wa amani, A4P, ulianzishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mwezi Machi mwaka huu ili kuhakikisha operesheni hizo zina tija kwa pande zote husika.

Audio Credit:
Siraj Kalyango/ Anold Kayanda
Audio Duration:
1'50"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud